TAKRIBANI miaka 15 imepita tangu ilipotokea ajali katika kijiji cha
Idweli wilayani Rungwe mkoa wa Mbeya, iliyosababisha vifo vya watu
walioungua wakichota petroli kwenye gari lililopinduka.
Hata hivyo, tukio la namna hiyo limejirudia tena kijijini hapo na
safari hii watu wawili, wamekufa na wengine 18 kujeruhiwa wakati
wakichota mafuta kwenye gari lililopinduka. Lori hilo lilikuwa
likisafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda Malawi.
Lilipinduka kijijini hapo juzi. Vifo hivyo viwili vya wakazi wa
kijiji hicho, Maria Pajela (18) na Wiliam Pascal (38), vimetonesha
makovu ya huzuni ya ndugu na jamaa wapatao 40 waliopoteza maisha na
kulazimu miili yao kuzikwa kaburi moja, kutokana na kuharibika zaidi na
kushindwa kutambuliwa.
Akitoa taarifa juu ya ajali ya juzi saa 3 usiku, Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema waliofariki na waliojeruhiwa,
walikuwa katika harakati za kuiba mafuta kutoka katika gari aina ya
Scania lenye namba za usajili T 891 AQZ likiwa na tela lenye namba T 821
ARF.
Alisema gari hilo mali ya Ailis Sanga, lilipakia petroli yenye ujazo
wa lita 41,000, likitoka Dar es Salaam kwenda Malawi. Lilikuwa
likiendeshwa na Zawadi Nyato (46) mkazi wa Sae jijini Mbeya akiwa na
utingo wake, Frank Yohana (24) mkazi wa Mbozi.
Baada ya kufika kijijini hapo, liliacha njia na kupinduka. Dereva na
utingo waliokolewa na kupelekwa kituo cha Polisi Kiwira kupata fomu
namba tatu ya kwa ajili ya matibabu.
Kamanda alisema baadhi ya wakazi, walivamia lori hilo na kutoboa
tangi la mafuta, hali iliyosababisha mafuta kuanza kumwagika na kusambaa
maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye makazi ya watu.
Kwa mujibu wa kamanda, watu hao hawakujali hatari iliyokuwa
ikiwakaribia, badala yake waliendelea kukinga mafuta kwa kutumia vyombo
vyao zikiwemo ndoo, madishi, karai na madumu.
“Wakati wakiendelea na harakati za wizi huo,wakazi hao walijikuta
wakiwa katika moto mkubwa baada ya lori hilo kulipuka na hapo ndipo
wawili kati yao wakapoteza maisha na waliosalia kujeruhiwa vibaya,”
alisema Kamanda.
Alitaja majeruhi katika ajali hiyo, ambapo wanaume ni 13 na wanawake
watano ni Shukuru Kanzale (21), Nuru George (30), Asante Boniface (38),
Joseph Jamson (18), Joseph Paschal (30), Siza Kanesa (22),Alex Daud
(35), Oscar Yosia (23), Traiphon Moasi (37) na Samson Mbwila (29).
Majeruhi wengine ni Veronica Elia (30), Dora Michael(35), Rabsen Ayub
(26), Wasiwasi Spika (32), Asia Anon (20), Bahati Kyando
(23),Christopher Erasto(32) na Melisa Sanane (50) wote wakazi wa kijiji
cha Idweli.
Kati ya majeruhi hao, 16 wamelazwa katika Hospitali ya Misheni Igogwe
na wawili wamelazwa Hospitali ya Serikali Makandana, Tukuyu na hali zao
zinaendelea vizuri.
Katika tukio la mwaka 2000 katika kijiji hicho cha Idweli, gari
lililohusika lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Malawi. Lilianguka
kijijini hapo, kutokana na utelezi katika mteremko unaoishia kwenye
kijiji hicho.
Tukio lingine la watu kuungua moto nchini, kutokana na kutaka
kujipatia mafuta ya bure, lilitokea mwaka jana katika eneo la Mbagala
Rangi Tatu, jijini Dar es Salaam la mwaka 2014.
Watu wanne walipoteza maisha na wengine 21 kujeruhiwa vibaya baada ya
kwenda kuchota mafuta yaliyokuwa yanamwagika wakiwa na ndoo, vidumu vya
lita tano na vyombo vingine bila kuchukua hadhari.