MKUU wa Wilaya ya Kinondoni , Paul Makonda (pichani) amesema
wanaobeza uwezo wake kiutendaji baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya
Kikwete kushika wadhifa huo, wasubiri waone atakavyokuwa.
Aidha, ameweka wazi kile anachoamini anashutumiwa na kubezwa na watu
kuhusu uteuzi huo na kusema wanaofanya hivyo, wanafahamu kwamba masuala
yao kadhaa ndani ya wilaya hiyo yanayokwenda kinyume na taratibu,
hayatafanikiwa.
Akiendelea kujibu wanaoshutumu uteuzi wake kupitia mitandao ya
kijamii na vyombo vya habari, alisema kwa sasa hawezi kutoa ahadi ni
nini atafanya isipokuwa, anasubiri kuingia ofisini.
Akihojiwa katika kipindi cha asubuhi cha Redio ya Clouds, alisema pia
anamsikiliza Rais atakachomwambia afanye kwa kuwa yeye ni mwakilishi
wake wilayani humo.
Akizungumzia kuhusu taarifa za kupata nafasi hiyo kuwa gumzo katika
jiji kuliko wakuu wengine wa wilaya, alisema inaonesha ni kwa jinsi gani
watu wanatambua utendaji wake.
Alisema alipata taarifa za uteuzi huo wakati akitoa mada katika kikao
cha kazi cha Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na
kushangaa watu wakipeana taarifa.
“Kuna watu wanabeza uteuzi wangu kwa kuonekana nimepewa wilaya kubwa.
Nataka kuwaambia wasubiri waone tu,” alisema na kutaka Watanzania
kuacha tabia ya kumjadili mtu au jambo bila kufahamu vizuri.
Alisisitiza kuwa Watanzania wamekuwa na tabia ya kushabikia jambo
wasilolijua au mtu wasiyemjua kwa kufuata mkumbo; jambo ambalo siyo zuri
ni vyema kufahamu kwanza ndipo uweze kusema.
Akizungumzia baadhi ya vyombo vya habari vilivyotoa taarifa za uteuzi
wake kwa kumdhihaki, alisema wamefanya hivyo kwa maslahi yao ya kuuza.
Pia alielezea uteuzi wake umekuwa gumzo, kutokana na uwezo wake wa
kazi katika UVCCM pamoja na uwezo wake kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Uteuzi wa Makonda ambao umefanywa na Rais Kikwete, unaonesha
kuwashitua wengi; hali ambayo imefanya watu wengi kumbeza hasa kupitia
mitandao ya kijamii.
Baadhi ya wanaobeza, wanadai kwamba Makonda hana sifa ya kuongoza
wilaya kubwa kama Kinondoni, ambayo ina changamoto na migogoro mingi ya
ardhi.
Makonda ambaye ni Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa UVCCM, jina
lake limekuwa kubwa hivi karibuni baada ya kutuhumiwa kushiriki kuvuruga
mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, tuhuma
alizokanusha.
Pia, kujitokeza kwake hadharani kumpinga mmoja wa watu wanaotajwa
kuwania urais, kuliongeza jina hilo kuwa maarufu. Maisha ya Makonda pia
ambaye baada ya kushindwa Umakamu Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM, alitoa
shutuma kuhusu uchaguzi huo na baadaye alirejeshwa ndani ya umoja huo
kwa kupewa nafasi anayoshikilia sasa ya ukatibu wa uchipukizi na
uhamasishaji.