Wabunge
wametaka kuwepo na udhibiti wa ongezeko la watu nchini kwa kutaka
wanaume wadhitibiwe katika uzazi, kama ilivyo kwa wanawake huku wengine
wakitaka serikali kuboresha rasilimali bila kudhibiti uzazi.
Miongoni
mwa waliotaka wanaume wafungwe kizazi kama inavyofanyika kwa wanawake
ni Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki, Celina Kombani ambaye pia ni
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Wakichangia
mada katika semina ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 kwa
wabunge, iliyoandaliwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) walisema ni vyema
kuwa makini katika kudhibiti uzazi, kwani inaweza kusababisha athari za
baadaye kuwa na wazee wengi kuliko vijana.
Mbunge
wa Dole, Sylvester Mabumba (CCM) alisema hakuna haja ya kuogopa
kuongezeka kwa watu, bali rasilimali zitumike vizuri kwa kutunga sheria
maalumu ya kubana mafisadi kwa kuwafilisi.
Mbunge
wa Arumeru Magharibi, God ole Medeye alishauri kuwa si vyema kudhibiti
uzazi, kwani kuna nchi walifanya hivyo sasa wamebaki na wazee tu hivyo
ni vyema kuangalia hali ya uchumi na uzazi.
Kombani
alisema kumekuwa na suala la uzazi wa mpango kwa wanawake tu, hivyo
katika kudhibiti idadi ya watu ni vyema wanaume nao wakadhibitiwa kwa
kufungwa uzazi.
Alisema ikiwa familia inataka kudhibiti kuzaa ni vizuri mwanamke akifunga kizazi na mwanamume naye afunge kuzaa.
Huku
akiungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM) aliyesema
ni vyema kudhibiti wanaume katika uzazi kwa kuwa na idadi sawa kati ya
wanawake na wanaume.
Mbunge
wa Rungwe Magharibi, Profesa David Mwakyusa alisema kuwadhibiti wanaume
ni jambo la muhimu, kwani iwapo mwanamume atakuwa amechepuka mara 100
atazaa watoto 100, lakini mwanamke akichepuka mara 100 atazaa mtoto
mmoja.
Mbunge
wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) alisema kudhibiti kuzaa ni kupinga
vitabu vya dini vilivyosema kuzaana sana kwani kila mtoto anakuja kwa
riziki yake huku akibainisha wazi kuwa ana watoto 12 na anatarajia
kufikisha 20 kwani kuna faida wapo wenye uwezo tofauti.
Mbunge
wa Mkuranga, Adam Malima (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha,
alisema ni vyema kuangalia mifano ya Japan na Norway na pengine
walipodhibiti uzazi na sasa wanaona athari yake, hivyo ni vyema
kuwaachia wataalamu kupata uwiano wa kuzaa idadi ya watoto wanaotakiwa
kuzaliwa.
Akihitimisha
majadiliano hayo, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema tatizo la
ongezeko la watu nchini ni kubwa na lazima kujipanga kudhibiti uzazi,
kwani itapunguza masuala mbalimbali.
Alisema
ukizaa watoto wachache ni lazima mke na watoto kuwa na afya njema huku
huduma za elimu na afya kuwa njema, kwani hata China walidhibiti uzazi
na sasa wanalegeza masharti baada ya kuona matunda yake, kwani ardhi
haiongezeki bali watu wanaongezeka.
Akifungua
semina hiyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitaka wabunge kuhakikisha
ongezeko la watu nchini, linaendana na ukuaji wa uchumi wa asilimia 7
kwa muongo mmoja.
Alitaka
kuhimiza matumizi bora ya uzazi wa mpango katika kaya, Sera ya Idadi ya
Watu na Makazi mwaka 2006 haina budi katika suala la ongezeko la watu.