Baadhi
ya hoteli za kitalii mjini Arusha zimefungwa, huku mishahara ya
wafanyakazi ikipunguzwa kwa asilimia 25, kutokana na kukosa watalii.
Akizungumza
wakati wa tafrija ya kuukaribisha mwaka mpya 2015, zilizoandaliwa na
Chama cha Mawakala wa Watalii Nchini (TATO), Mwenyekiti wa chama hicho,
Willy Chambulo alisema hali ya biashara kwa miezi hii mbaya na
kusababisha kufungwa kwa baadhi ya hoteli.
Alisema: “Mimi
mwenyewe hoteli zangu sita nimezifunga na baadhi ya wenzangu pia
wanatarajia kufunga hoteli zao kwa sababu ya kukosa watalii.”
Pia
alitoa ombi kwa serikali wakati huu wa ukosefu wa wageni ni vyema
wakapunguziwa nusu ya bei kwa viingilio na kodi za serikali wanazotoza
kwa kuingia nchini na hifadhini.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alikubaliana na ombi hilo huku akisema: “Kutokana
na hili, sisi Tanzania tumelisikia hili tatizo, hivyo hatutaongeza bei
yoyote na ndiyo sababu Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) pia
hatujaibebesha sekta ya utalii, ili kuwapunguzia mzigo.”
Nyalandu
alisema Serikali pia haitaongeza tozo yoyote ya kuingilia hifadhi za
taifa hasa katika kipindi hiki cha upungufu wa wageni.
Alisema
kila mwaka Tanzania imekuwa ikipokea watalii 250,000 wanaopitia Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya, hivyo tishio la
ugaidi kwa nchi hiyo, kumeleta shida pia kwa kupunguza watalii nchini.
Naye
Mkurugenzi wa Kampuni ya kitalii nchini ya Leopard, Zuhel Fazal alisema
kwa kampuni yao wamepunguza mishahara kwa asilimia 25.