TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema katika majaribio ya
uandikishaji wananchi kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, mfumo
mpya wa uandikishaji wa ‘Biometric Voter Registration Kit’ (BVR),
umefanikiwa kwa asilimia kubwa licha ya changamoto kadhaa, na ina
uhakika mfumo huo utatumika kuwaandikisha Watanzania wote katika daftari
hilo bila matatizo.
Aidha, Tume hiyo imebadilisha tarehe ya kuanza rasmi uandikishaji wa
wananchi katika daftari la kudumu uliokuwa uanze Februari 16, katika
mkoa wa Njombe, hadi Februari 23, mwaka huu, ili kutoa nafasi kwa wadau
kuweza kujiandaa vyema.
Pamoja na hayo, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, wameonesha
wasiwasi juu ya utaratibu mzima wa uandikishaji wananchi katika daftari
la kudumu kupitia BVR, kuwa kama utafanyika na kumalizika kwa wakati,
kutokana na tume hiyo kuchelewa kufanya mambo mengi, ikiwemo elimu ya
uraia na kutoa ratiba ya uandikishaji.
Akifungua mkutano ulioandaliwa na tume hiyo kwa ajili ya kukutana na
vyama vya siasa kujadili uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura,
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Damian Lubuva, alisema tume hiyo ilianza
utaratibu wa majaribio ya uandikishaji kwa kutumia mfumo huo katika
mikoa mitatu ambayo ni Dar es Salaam, Morogoro na Katavi.
“Kwa ujumla uandikishaji ulifanyika vizuri na kwa mafanikio katika
maeneo yote, idadi ya watu walioandikishwa pia katika maeneo hayo
iliongezeka na kuvuka lengo ambalo tume iliweka kwa zaidi ya asilimia
100 licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa, hii ni dalili nzuri kwamba
mfumo huu utafanikiwa,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema tume hiyo katika eneo la Kawe mkoani Dar es Salaam ililenga
kuandikisha wananchi 14,312, lakini waliandikishwa wananchi 15,123 sawa
na asilimia 105.67, Kilombero mkoani Morogoro waliandikishwa wananchi
19,188 wakati lengo la Tume lilikuwa wananchi 17,290 sawa na asilimia
110.9.
“Pia katika mkoa wa Katavi, wilayani Mlele, tuliweka lengo la
kuandikisha wananchi 11,104 lakini kupitia mfumo huu wa BVR ambao katika
kila kituo tulitumia BVR kit 80, tuliandikisha wananchi 11,210,”
alisisitiza.
Aliwahakikishia wanasiasa hao kuwa, kutokana na majaribio ya mfumo
huo katika mikoa hiyo, pamoja na kubaini changamoto kadhaa, tume hiyo
ina uhakika mfumo huo ni imara na unaweza kutumika kuandikishia
Watanzania wote katika muda uliopangwa bila matatizo.
Hata hivyo, alisema tume hiyo imebadilisha muda wa kuanza
uandikishaji kutoka Februari 16 hadi 23, mwaka huu, ambapo katika mkoa
wa Njombe pekee wanatarajia kutumia vifaa vya BVR takribani 250 huku
vifaa vingine 7,050 vikisubiriwa kuwasili nchini kwa ajili ya
uandikishaji kuendelea maeneo mengine.
“Suala la ratiba tunalifahamu na tutaitoa muda wowote, tayari
Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya vifaa hivi ambavyo vinatokea
China, awamu ya kwanza vifaa takribani 2,000 vitawasili wiki ya kwanza
ya mwezi Machi, napenda nitoe wasiwasi, Tume iko huru, wazi na haina
chochote inachokificha wala kutumika na mtu,” alisema.
Aidha, Jaji Lubuva, alisema kutokana na taarifa za sensa, tume hiyo
imeongeza vituo vya uandikishaji wapiga kura kutoka vituo 24,919 vya
zamani hadi vituo 36,109.
Naye Mkurugenzi wa tume hiyo, Julius Malaba, alisema katika majaribio
ya mfumo huo wa BVR, changamoto kadhaa zilijitokeza ikiwemo mfumo mzima
wa BVR ulivyoandaliwa (setting), hardware na programu zinazotumiwa na
mfumo huo pamoja na maeneo ya uendeshaji uandikishaji huo.
“Changamoto zote hizi tumezifanyia kazi kwa kuzirekebisha. Katika BVR
zitakazotumika mkoani Njombe nazo zimefanyiwa marekebisho kutokana na
changamoto zilizojitokeza, ila tumechukua tahadhari za uhakika ili
kuhakikisha utaratibu mzima unafanyika bila tatizo,” alisema Malaba.
Wakitoa maoni yao kuhusu mada hiyo, wengi wa viongozi wa vyama vya
siasa walionesha wasiwasi na tume hiyo kwa kushindwa kuwasilisha ratiba
nzima ya uandikishwaji nchi nzima ikiwa ni pamoja na utaratibu huo
kuanza huku vifaa vingi vikiwa bado havijawasili.