SIKU chache baada ya Serikali kusema itazifutia usajili shule
zitakazokaidi agizo la kuweka viwango maalumu na tofauti vya ufaulu
kutoka kidato kimoja kwenda kingine, wadau wa elimu wamezungumza na
kusema agizo hilo linalenga kuua ubora wa taaluma nchini.
Akizungumza na HabariLeo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki na
Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), Benjamin
Mkoya alisema viwango vinavyowekwa na shule binafsi vinakubaliwa na
wazazi na kuwa kinyume chake shule hizo zitakufa kutokana na uwezekano
wa kufifia ubora wa kitaaluma.
“Viwango vinavyoweka huwa vinakubaliwa na wazazi, na lengo la kufanya
hivyo ni kutaka shule zifanye vizuri hivyo kuweza kujiendesha, kwani
mbali na kutoa huduma, tunafanya biashara,” alisema Mkoya.
Alisema suala la baadhi ya shule kupanga viwango vya ufaulu limekuwa
likifanyika muda mrefu na kuridhiwa na wizara husika ya elimu Julai
2013, baada ya agizo la kuifungia shule ya sekondari ya Mwilavya, Kasulu
mkoani Kigoma iliyopandisha viwango vya ufaulu hadi kufikia asilimia 45
kutokana na matakwa ya wazazi.
Mkoya alisema suala hilo lilifika wizarani na uongozi wa TAMONGSCO
kukutana na Naibu Waziri (wakati huo akiwa ni Philipo Mulugo) ambaye
alisema kama wazazi wameridhia viwango hivyo, shule zinatakiwa kuendelea
kufuata viwango hivyo.
“Tulikutana na uongozi wa wizara, na hapa hatumuangalii mtu
aliyekuwepo ofisini bali taasisi,” na tulizungumza hilo, na hapo
walisema kama wazazi wanaridhia viwango hivyo basi hakuna sababu ya
kugombana na wapiga kura ambao wanataka viwango vya juu,” alisema na
kuongeza kuwa kwa mwaka huu pekee wameshafanya vikao na viongozi wa
Wizara ya Elimu mara mbili kwa lengo la kuboresha sera ya elimu na suala
zima la Matokeo Makubwa Sasa (BRB).
Aidha, Mkoya alisema Serikali imekuwa ikitoa maagizo mbalimbali
yanaonekana kulenga kudhoofisha shule zisizo za serikali, na kutolea
mfano wa agizo lililotangulia lililotolewa na TAMISEMI likizitaka shule
hizo kutosajili wanafunzi mpaka hapo shule za serikali zitakapojaa.
“Serikali inatakiwa kutoona shule hizi kama ni ebola na kuzipiga
vita, badala yake wazione kama partner (mshirika) katika kuboresha elimu
hasa katika kufikia BRN. Mkoya alisema wakati umefika sasa, sekta ya
elimu kuwa na taasisi huru ambayo itasimamia elimu hapa nchini hivyo
kuondoa mgongano wa kimaslahi kutoka kwa serikali ambayo ni wamiliki wa
shule na pia ndio wanaosimamia elimu. “Tunataka mamlaka huru kama ilivyo
SUMATRA, Wizara ndio yenye shule na ndio inayosimamia elimu, hapa
hapatakuwa na usawa,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Huduma ya Elimu kwa Tume ya Kikristo ya Huduma za
Jamii (CSSC) ambayo ni Bodi ya muungano wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo (CCT), Petro Pamba alisema shule
zao hazitakwepa mfumo wa kupanga viwango vya ufaulu kwani unaandaa
wanafunzi na uwajibikaji kwa walimu.
Alisema taasisi yake yenye shule za sekondari 368 nchi zima imekuwa
ikiendesha shule kwa mifumo miwili ambayo ni shule za seminari ambayo
zinalenga kuwaandaa watumishi wa kanisa na ile ya kutoa huduma ya elimu
kwa jamii.
Alisema mfumo wa kupanga viwango vya ufaulu umekuwa ukitumika muda
mrefu na kujulikana na wizara na kwa sasa hawawezi kuukwepa kwani
umekuwa ukiwaandaa vizuri wanafunzi na uwajibikaji kwa walimu.
“Mfumo wa kuweka viwango vya ufaulu unawafanya walimu pia
wajitathmini, ukiwaacha walimu huru basi nao wanabweteka, hivyo sisi
tutaendelea na mfumo huo kwani umekuwa ukifanyika muda mrefu na mamlaka
za elimu zinaelewa,” alisema.
Alisema viwango vilivyopo sasa ni kati ya asilimia 40 hadi 49 na kuwa
zaidi ya asilimia 50 kwa shule za seminari ambazo zinaandaa watumishi
wa kanisa.
“Huko kwenye seminari mchujo wetu ni mkali sana kwa sababu ndio
tunaowaandaa watumishi ambao watakuwa wakihudumia jamii hivyo kutakiwa
wawe vizuri kichwani,” alisema.
Hata hivyo, Pamba alisema taasisi yao inakamilisha mfumo mbadala wa
kuwasaidia wanafunzi wanaoelewa taratibu kwa kuwaandalia mafunzo maalumu
ili waweze kufanya vizuri mitihani ya mwisho na kuwa wale wenye alama
za chini watalazimika kurudia darasa.
Alisema pamoja na Wizara kutaka shule kufuata Sera ya Elimu inayotaka
viwango vya ufaulu kuwa ni asilimia 30, alisema sera hiyo inaelekeza
kwa wanafunzi wanapotakiwa kuvuka kutoka kidato cha pili kwenda cha tatu
na si katika madarasa mengine.
Alisema pia kiwango hicho cha ufaulu ni cha chini ukilinganisha na
mfumo mpya wa upangaji wa alama za ufaulu unaofanywa na Baraza la
Mitihani Tanzania (NECTA) ambayo ufaulu ni kati ya alama 40 hadi 49 (C),
huku alama 30 hadi 39 ni ufaulu hafifu ambao unatoa daraja D.
Alisema kutokana na alama hizo kupitwa na wakati, CSSC, imepeleka
pendekezo wizarani kutaka kubadilishwa kwa viwango vya ufaulu hadi
kufikia alama 40 kwa kidato cha pili kwenda cha tatu.
Alipoulizwa Katibu wa Elimu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA)
Mohammed Jongo alisema: ”Wizara ndio wasajili wa shule hapa nchini hivyo
tutatekeleza agizo lao.”
Kwa nyakati tofauti wakijibu maswali bungeni, Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na Naibu wake Anne Kilango
Malecela walisema serikali itazifutia usajili shule zote za serikali au
binafsi, zitakazobainika kukaidi agizo la kuacha kuweka viwango maalumu
na tofauti za ufaulu kutoka kidato kimoja kwenda kingine.
Waraka wa Elimu Namba 6 wa mwaka 2011, umetoa maelekezo kuhusu
wastani wa ufaulu katika mtihani wa kidato cha pili ambapo kiwango cha
alama ya ufaulu ni asilimia 30 tu na si vinginevyo kwa shule za serikali
na binafsi.