Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal jana aliwaongoza mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, kuzika miili ya watu sita wa familia moja waliokufa katika ajali ya moto wakiwa nyumbani kwao Kipunguni, Manispaa ya Ilala usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.
Katika
maziko hayo yaliyofanyika makaburi ya Airwing yaliyopo Ukonga Banana,
ibada ya maziko iliongozwa na Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo
Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigirwa akisaidiwa na mapadri watano.
Umati
wa wananchi ulianza kufurika mapema, ingawa shughuli ya kuihifadhi
miili ya marehemu hao ilianza saa 7:08, baada ya kuwasili kwa Makamu wa
Rais na kuendelea kwa saa sita mfululizo hadi takribani saa moja usiku.
Makaburini
hapo, majeneza sita yalipangwa kila moja karibu na kaburi, huku baba wa
familia, David Mpira akitangulia kuzikwa kwa kutanguliza kiungo cha
mguu wake kilichotambuliwa jana asubuhi chumbani kwake na baadaye
kuwekwa jeneza na kuzikwa rasmi.
Mpira,
aliyekuwa askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), hadi
mauti yanamfika alikuwa Katibu wa kikundi cha wanamaombi wa kanisa hilo.
Baadaye
alizikwa mke wa Mpira, Celina Yegela (50) aliyekuwa mstaafu wa Shirika
la Usafirishaji Mizigo kwa Njia ya Ndege (DAHACO). Wengine waliokufa
katika ajali hiyo na kuzikwa jana ni Samuel Yegela aliyekuwa anajiuguza
nyumbani kwa dada yake, Lucas Mpira mtoto wa familia hiyo na wajukuu
wake, Celina na Paulina Emmanuel.
Ndugu
wa marehemu, wakiongozwa na mtoto pekee wa familia hiyo aliyenusurika,
Emmanuel Mpira, baba wa watoto wawili waliokufa ambaye amepoteza pia
wazazi wawili, mjomba na kaka yake, waliangua vilio vya mara kwa mara
huku baadhi yao wakipoteza fahamu.
Awali,
mara baada ya kuwasili kwa miili yao, Makamu wa Rais aliongoza kutoa
heshima kwa marehemu hao kwa kuangalia picha zao, akifuatiwa na Askofu
Nzigirwa, Mawaziri Profesa Mark Mwandosya na Dk Harrison Mwakyembe,
Naibu Waziri Dk Milton Makongoro Mahanga, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Said Mecky Sadiki, wanafamilia na baadaye waumini wachache
waliowakilisha umati wa wananchi waliohudhuria.
Katika
ibada hiyo, Askofu Nzigirwa alitoa salamu kutoka Jimbo Kuu la Dar es
Salaam na kusema msiba huo ulikuwa mzito, kutokana na kuondoa familia
yote kwa wakati mmoja, huku akisema majibu ya maswali waliyonayo watu
wengi yapo kwa Mungu.
“Tumesikia
kuwa vifo hivi vimetokana na ajali, hivyo tunajiuliza kwa nini
wasingeacha kuangalia televisheni wasingekufa au vikosi vya ukoaji
wangewahi wasingekufa, ni vyema kuacha kujiuliza kwa nini, bali tumuombe
Yesu awapokee katika ufalme wake,” alisema.
Alisisitiza
kuwa, familia hiyo ilikuwa ikiishi kwa kumtumainia Mungu na kwamba hata
kama walikuwa na mapungufu yao, lakini hawakumwacha Mungu, hivyo tukio
hilo la kuchukua familia na watu wa rika tofauti, linafundisha jamii
kuishi kwa kumtumikia Mungu.
Makamu
wa Rais, akizungumza katika maziko hayo, alisema msiba huo ni mkubwa na
aliwapa pole wafiwa na kuwaomba kuwa na moyo wa subira huku akiwaombea
marehemu miili yao ilale mahali pema peponi.
Aliwasihi
Watanzania kujitahidi katika nyumba zao kuwa na vizimia moto na
kuhakikisha wanajitahidi kuweka madirisha au milango ya dharura kwenye
nyumba zao.
Aliwataka wakati wa matukio ya moto, kuhakikisha wanapiga namba ya zimamoto 114 badala ya kupiga namba za polisi.
Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal akiweka shada la maua.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam akiweka shada la maua.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya akiweka shada la maua.
Jaji Mkuu mstaafu, Agustino Ramadhani akiweka shada la maua.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib
Bilal akitoa heshima za mwisho kwenye majeneza yenye miili ya Familia ya
marehemu Kapten David Mpila waliofariki kwa kuteketea na moto nyumbani
kwao Kipunguni, wakati wa mazishi yao yaliyofanyika Februari 10,2015
katika makaburi ya Airwing Ukonga Dar es salaam.