SERIKALI YAANZA KUSAMBAZA KWA WANANCHI KATIBA INAYOPENDEKEZWA


Serikali imeanza kusambaza nakala milioni mbili za Katiba Inayopendekezwa nchini kote ili kuwawezesha wananchi kuisoma na kushiriki katika Kura ya Maoni iliyopangwa kufanyika tarehe 30 Aprili mwaka huu.

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro amesema JANA (Jumatano, Februari 11, 2015) jijini Dar es Salaam kuwa kati ya nakala hizo zilizochapwa jijini Dar es Salaam, nakala 1,800,000 zinasambazwa Tanzania bara na nakala 200,000 zinasambazwa Tanzania Zanzibar.

Kwa mujibu wa Waziri Migiro, hadi kufikia jana (Jumanne, Februari 10, 2015), jumla ya nakala 707,140 zilikuwa zimesambazwa katika mikoa 12 ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ambayo imepata nakala 200,000 na kuwa kazi hiyo inaendelea vizuri na inatarajiwa kukamilika katika muda mfupi ujao.

Mikoa hiyo na nakala ziliozosambazwa katika mabano ni Katavi (15,640), Rukwa (27,040), Ruvuma (47,740), Mbeya (78,640), Simiyu (34,840), Mara (52,540), Tabora (58,540) na Kigoma (41,440). Mikoa mingine ni Kagera (54,340), Geita (36,940), Mwanza (57,040) na Pwani ambapo usambazaji umeanza kwa wilaya ya Mafia ambayo imepata nakala 2,400.

“Idadi ya nakala ya Katiba Inayopendekezwa kwa kila mkoa inategemea na wingi wa kata katika mkoa, ndiyo maana baadhi ya mikoa unaona imepata nakala nyingi,” amesema Dkt. Migiro ofisini kwake wakati akiongea na baadhi ya waandishi wa Habari waliotaka ufafanuzi kuhusu hatua iliyofikiwa katika kazi ya uchapishaji na uasambazaji wa nakala za Katiba Inayopendekezwa.

Kwa mujibu wa Waziri Migiro, kuna zaidi kata 3,800 nchini kote na lengo la Serikali ni kusambaza nakala 300 katika kila kata ambazo zitasambazwa kwenye vijiji, vitongoji na mitaa kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji.

Kuhusu taasisi za elimu na dini, Waziri Migiro amesema Serikali imepanga kusambaza nakala 658,400 kwa taasisi za elimu, dini, vyama vya siasa na asasi za kiraia na kuwa usambazaji huo utaanza hivi karibuni.

Pamoja na usambazaji huo, Waziri Migiro amewakumbusha wananchi ambao bado hawajapata nakala za Katiba Inayopendekezwa, kuisoma kupitia tovuti ya Wizara ya Katiba na Sheria (www.sheria.go.tz) na tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (www.agctz.go.tz).


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo