Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Ilola, Kata ya Ilola Itwangi,
Wilaya ya Shinyanga Vijijini, mkoani hapa, mwenye umri umri wa miaka 12
(jina lake linahifadhiwa kutokana na umri wake), anashikiliwa na polisi
kwa tuhuma za kumuua mwenzake kwa kumpiga ngumi kichwani na kuangukia
kisogo, wakati wakigombea daftari waliloazima.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Longinus Tibishubwamu,
jana alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 7:30 mchana na kwamba,
wanamshikilia mwanafunzi huyo kwa mahojiano na kwamba wakikamilisha
upelelezi atafikishwa mahakamani.
Alimtaja mwanafunzi aliyefariki dunia kuwa ni Veronica Venance (12), aliyekuwa anasoma darasa moja na mwezake aliyesababisha kifo hicho.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Magere Jonas, alisema wakati wanafunzi hao wanagombea daftari hilo, alikuwa amepumzika chini ya mti akiwa na mwalimu mkuu msaidizi.
Jonas alisema baada ya kuingia darasani,
walimkuta mwanafunzi huyo akiwa amelala chini akigalagala, hivyo
kumkimbiza kwenye kituo cha afya Bugisi kilichoko jirani na shule hiyo,
lakini kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo alifariki dunia.
Mtendaji wa Kata ya Ilola, Mahona Joseph,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza marehemu alikuwa
ameng’anga’nia daftari alilokuwa ameazimwa na Sophia Mathew kwa ajili ya
kuandika ‘notes’ kitendo ambacho kilimkera mwenzake na kuzua ugomvi.
“Tunahisi
kifo cha mwanafunzi huyu kilitokana na kuanguka vibaya mara baada ya
kusukumiwa ngumi na kukipiga kisogo, hivyo kukata mawasiliano na
kusababisha kifo chake. Masuala mengi tumeviachia vyombo vya sheria”;-Joseph