Mamia ya wakazi wa Makete wamejitokeza kumzika aliyekuwa mchungaji kiongozi
wa usharika wa Lupalilo marehemu Nazeth Luvanda aliyefariki Dunia Februari
11mwaka huu
Akihubiri katika ibaada hiyo ya mazishi iliyofanyika katika makaburi ya
Mwongolo katika mji mdogo wa Iwawa, Askofu dayosisi ya kusini kati Levis Sanga
amewaasa watu kuishi kwa kumpendeza Mungu katika maisha yao kwa kuwa kifo
kitamchukua kila mtu bila kujua
Askofu Sanga amesema katika maisha mafupi tunayoishi hapa duniani ni vema
kila mmoja kukumbuka kuishi maisha ya uchaji na yenye kumpendeza Mungu kila
wakati, ili kila mmoja atakapofikwa na umauti akaurithi uzima wa milele
Katika maziko hayo zilitolewa salamu za rambirambi kutoka kwa ndugu jamaa
na marafiki wa marehemu kabla ya viongozi na wananchi walioshiriki maziko hayo
ya Mchungaji Luvanda kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu
Marehemu Mch. Luvanda alizaliwa 19.04.1955 wilayani Mufindi na kufanya
shughuli za uchungaji toka alipobarikiwa kama mchungaji mwaka 1985 kazi ambayo
aliifanya katika vituo mbalimbali alivyopangiwa ikiwemo usharika wa Luwumbu,
Usharika wa Mbanga, mkuu wa jimbo la Ludewa wakati huo likiitwa eneo la
Misioni, usharika wa Idunda, Mwenyekiti wa uamsho na maombi ndani ya dayosisi
na Mchungaji kiongozi usharika wa Lupalilo hadi mauti inamkuta
Marehemu Mchungaji Nazareth Luvanda ameacha mjane mmoja, watoto 6 pamoja na
wajukuu wanne, na Mungu alaze mahali pema peponi roho ya marehemu.