Afisa
Habari wa Bodaboda Wilaya ya Ilala, Abdallah Bakari ‘Dullah’
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar.
Na Andrew Chale
Waendesha
Bodaboda Wilaya ya Ilala wamepanga kuandamana hadi Ikulu kuonana n Rais
kwa ajili ya kutoa malalamiko yao dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji, Meya na
Mkuu wa Mkoa kwa kile wanachodai viogozi hao kushindwa kudhibiti vitendo
vya manyanyaso wanavyofanyiwa na askari mgambo wa jiji ambao wamekuwa
wakiwakamata pamoja na kupora Pikipiki zao.
Akizungumza
na waandishi wa habari mapema leo, Afisa Habari wa Bodaboda Wilaya ya
Ilala, Abdallah Bakari ‘Dullah’ ambaye jana alikumbwa na adha ya askari
mgambo hao waliomkamata na kumpiga kwa kile walichodai alikuwa akiuza
matunda katikati ya jiji, eneo la Posta.
Akifafanua
juu ya kusudio lao hilo la kuandamana ambapo alibainisha kuwa, askari
hao Mgambo wamezidi kuwa kero kwao hasa bodaboda zilizopo katikati ya
jiji, ambapo hadi kukamatwa kwake na kisha kupigwa na kuporwa
vitambulisho na leseni zake, ni mara baada ya kuwatetea wenzake wa
bodaboda waliokuwa wamekamatwa na askari hao.
Akielezea
tukio hilo, “Wakati akimtetea bodaboda, eneo la Posta jirani na ofisi
za Idara Habari MAELEZO, watu watatu walimzingira mmoja wa bodaboda,
huku wakimshusha kwenye pikipiki yake. Mimi nikawahoji nyie wakina nani
kwa sababu hawana sare za kuwatambulisha wala vitambulisho, mimi nilitoa
kitambulisho changu kuwaonyesha wakanipokonya na kitambulisho pamoja na
leseni yangu wakanitia ndani ya gari ya Jiji ‘Site’ kama mwizi huku
wakinishambulia kwa kunipiga” alieleza Dullah.
Dullah
aliongeza kuwa, walimpeleka Mahabusu ya Jiji, ambapo alikaa hapo hadi
saa 12 jioni, ndipo alipowasiliana na Mkurugenzi wa Manispaa, alikana
kushughulika na suala hilo huku akimtaka awasiliane na Mkurugenzi wa
Jiji, lakini Mkurugenzi wa jiji hakuwa tayari kupokea simu, kwani hata
Meya wa Ilala kwa upande wake hakupatikana.
“Nilipowasiliana
na Naibu wa Wizara ya Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga, kumweleza
yaliyonikuta, lakini hakuweza kuchukua maamuzi yoyote, hivyo
nikawasiliana na viongozi wa bodaboda mkoa wa Dar es Salaam, akiwemo
Mwenyekiti Saidi Kagomba, ambao walifika na walihoji kwa nini
nimekamatwa, walijibiwa kuwa, Nimetukana na kosa lake ni faini sh
50,000/, nikapewa na kosa la kufanyabishara Posta ya kuuza matunda na
yule bodaboda niliyekuwa namtetea, hivyo tukatoa sh 50,000, na
kutolewa” alieleza Dullah.
Aidha,
Dullah alikemea vikali kitendo hicho huku akisema kwa sasa wameshakaa
vikao na kulaani vikali matukio hayo ya kinyanyasaji na wakati wowote
wataandamana hadi Ikulu kumuona Rais na kutoa malalamiko hayo ikiwemo
kukamatwa kila siku bila makosa, licha ya kutimiza masharti.
Aidha,
aliwaomba wanabodaboda wote wa Mkoa wa Dar es Salaam, kuungana kwa
pamoja kukemea matendo maovu wanayofanyiwa ikiwemo askari Mgambo wa
jiji, watu wanaokamatakamata ikiwemo wale wa Tambaza na wengineo hasa
wasio na vitambulisho ama sare maalum kutoa taarifa kwa viongozi wao
ikiwemo kuripoti Polisi ama kuwasiliana na namba 071376433, namba
ambayo ni ya afisa habari wa bodaboda.