Katika
hali isiyokuwa ya kawaida, mkazi wa mjini Namanyere mkoa wa Rukwa,
Gilbert Paul (37) aliyejiandalia maziko yake miaka 14 iliyopita, bado yu
hai.
Kwa sasa mtu huyo ameanza maandalizi ya kuchimba na kujenga kaburi la gharama, ikiwa ni pamoja na kununua jeneza.
Paul,
baba ya mtoto mmoja na mchoraji maarufu mjini Namanyere aliyehitimu
Kidato cha Nne 2001 katika Shule ya Sekondari Nkasi, anasema anafanya
hivyo kwa kuwa ana amani maisha ya duniani yana ukomo wake na ni ya
kupita tu.
Aliyasema
hayo juzi, akithibitisha kujichongea msalaba mkubwa na kuutundika
kwenye paa la kibanda chake anamofanyia kazi zake katika Mtaa wa
Sasala.
Msalaba
huo mweupe mkubwa, umeandikwa tarehe aliyozaliwa ya Desemba 24,
1977, lakini katika tarehe ya kufa, ameweka alama ya kiulizo. Msalaba
huo unaonekana waziwazi, kiasi cha wageni wanaopita eneo hilo, kudhani
ni nyumba ya ibada.
Paul
alisisitiza kuwa msalaba huo uliofikisha miaka 14 sasa, ndio
utakaosimikwa katika kaburi lake, ambalo anatarajia kulichimba na
kulijengea, akikadiria litamgharimu Sh milioni moja, sawa na gharama ya
jeneza alilotarajia kulinunua.
“Nilipotafuta
mafundi wanitengenezee msalaba huu, wote waligoma wakidai ni uchuro
na hawajawahi kusikia wala kuona mtu akijifanyia maandalizi yake
ya maziko akiwa bado anaishi .
“Mama
alilia sana walipomtaarifu, akidai katika ukoo wa baba yangu na wa
kwake hakuna aliyewahi kufanya hivyo …Baba alifariki nikiwa na miaka
saba, mwanzoni watu walidhani nina tatizo la akili na wengine
waliamini nimeathirika kwa Ukimwi hivyo nimekata tamaa ya kuishi, lakini
sivyo…“ anasema.
Alieleza
kuwa katika maisha yake yote, hakuwahi kuwa na rafiki wa kike mjini
humo kutokana na kujitengenezea msalaba huo, unaomfanya wamuogope
sana, hadi kuona kuna ulazima wa yeye kwenda kijiji cha mbali na hapo .
“Nilichumbia na kuoa chapuchapu nikihofia mke wangu mtarajiwa akibaini nimejitengenezea msalaba hatanikubali,“ alieleza.
Mke wa Paul, Paskaria Salvatory (25) akizungumzia tukio hilo, anasema kama angefahamu, kamwe asingekubali kuolewa naye.