Matukio ya wasafiri kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
wakiwa na nyara za Serikali na dawa za kulevya, yanazidi kuchukua sura
mpya baada ya raia mmoja wa Ubelgiji kukamatwa akiwa na fuvu la
binadamu.
Raia huyo, Balcjan Christine Weejktgns
(49) alikamatwa Jumatatu saa 2:30 usiku wakati akiwa katika taratibu za
kuingia uwanjani hapo tayari kwa safari ya kuelekea Ubelgiji kupitia
Zurich, Uswisi.
Tukio la kukamatwa kwa Mbelgiji huyo ni
mwendelezo wa matukio ya aina yake uwanjani hapo baada ya watu wengine
wawili kukamatwa kwa nyakati tofauti kwenye uwanja huo wakiwa na kucha
za simba na kenge walio hai.
Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege,
Hamisi Selemani alisema mtu huyo alikutwa ameficha fuvu hilo la binadamu
kwenye mfuko wa plastiki.
“Alivyopita
kwenye mashine za ukaguzi tulimtilia shaka na tulipompekua tulimkuta
amebeba fuvu la kichwa cha binadamu kikiwa kimewekwa kwenye mfuko wa
plastiki ndani ya sanduku alimokuwa ameweka nguo zake na vitu
mbalimbali:-Selemani.
Raia huyo anadaiwa kuwa ni mkazi wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro na inadaiwa kuwa alikuwa nchini kwa ajili ya kufanya utafiti.