Timu ya taifa ya Ghana imefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya
michuano ya Afcon baada ya kuwafunga wenyeji Equatorial Guinea katika
mchezo wa nusu fainali uliopigwa usiku huu (Alhamis).
Ghana wakiingia kwa kujiamini baada ya kuwatoa Guinea katika hatua ya
robo fainali walianza kuonyesha dhamira yao mapema wakishambulia lango
la wapinzani wao kwa nguvu na walipata bao mapema kwenye dakika 42
mfungaji akiwa Jordan Ayew ambaye alifunga kwa mkwaju wa penati baada ya
kipa wa Equatorial Guinea kumchezea vibaya Kwesi Appiah.
Ghana walifunga bao la pili kupitia kwa Mubarak Wakaso ambaye
alifunga kwenye dakika ya 46 baada ya kupokea pasi toka kwa Christian
Atsu .
Nahodha wa timu hiyo katika mchezo huo Andre Ayew ambaye alikuwa
anshikilia nafasi ya Asamoah Gyan alifunga bao la tatu kwenye dakika ya
75 na kuua matumaini ya Equatorial Guinea kucheza fainali .
Mchezo huo ulilazimika kusimama kwa muda baada ya mashabiki wa
Equatoarial Guinea kuanza kufanya vurugu wakionyesha hasira zao baada ya
kufungwa .
Ghana ambao wameingia kwenye fainali yao ya kwanza tangu mwaka 2010
watakutana na Ivory Coast katika mchezo wa fainali utakaopigwa jumapili
ijayo huku Equatorial Guinea wakicheza mchezo wa kuwania nafasi ya tatu
dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo siku ya jumamosi.