Polisi aliyejiua kwa kujipiga risasi mdomoni, Aloyce Mafuru (24), amezikwa katika makaburi ya Mugumu, Wilaya ya Serengeti, Mkoa wa Mara bila huduma za kidini na kijeshi.
Askari huyo aliyekuwa dereva wa Kamanda wa Polisi
Wilaya ya Manyoni, Alute Makita alijiua Februari 2 nyumbani kwake na
kuacha ujumbe kuwa polisi wasiangike kufanya uchunguzi kwani huo ni
uamuzi wake binafsi.
Paroko wa Kanisa Katoliki Mugumu, Padri Aloyce
Magabe jana aliwaeleza waombolezaji kuwa ingawa Mafuru alipata
kipaimara, lakini kujiua kumesababisha kanisa kushindwa kuendesha ibada
ya mazishi kwa kuwa kitendo hicho siyo mapenzi ya Mungu.
“Haifai kusema bwana ametoa na bwana ametwaa,
maana tendo alilofanya huyu halimtukuzi Mungu bali shetani, maana ni
kama ilivyofanyika kwa Kaini na Abel.
“Kaini alimuua ndugu yake na Mungu akamwambia
atubu dhambi, akawa mkaidi kwa sababu alikuwa na roho ya shetani na
matokeo yake alipata shida,” alisema Padri Magabe.
Aliwataka waombolezaji kushirikisha watu wengine
matatizo yao badala ya kujiua, kwa kuwa uamuzi wa kujiua ni matokeo ya
kutotafuta ushauri na kueleza kuwa tendo kama hilo linakosa utukufu kwa
Mungu.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Manyoni, taratibu za
mazishi ya kijeshi hufanywa kwa askari aliyeuawa, aliyeugua au
aliyepata ajali, lakini anayejiua hapewi heshima hizo.
“Kwa askari aliyejiua hawezi kupewa heshima hizo
kwa sababu anachukuliwa kama mwoga,” ilisema sehemu ya risala ya polisi
katika mazishi hayo.
Katika tukio jingine, kwa mila na desturi za
Kijita, maiti ya mtu aliyejiua haiingizwi ndani ya nyumba yake na badala
yake shughuli zote hufanywa nje.
Mama wa marehemu Elizabeth Dalali alisema hana taarifa zozote kuhusu chanzo kilichomfanya mtoto wake ajiue kwa risasi.
Dalali alisema maiti ya mwanaye haikuingizwa ndani
badala yake kilitengenezwa kibanda nje, kwani katika mila zao, kujiua
ni kitendo kinachoashiria mikosi.