Dereva bodaboda Ismail Lucas (16), mkazi wa Kwa Mathias wilayani Kibaha mkoani Pwani, anatuhumiwa kumlawiti mtoto ambaye ni mwanafunzi wa Chekechea.
Mama wa mtoto huyo (jina limehifadhiwa) alisema kuwa kutokana na tukio hilo, mwanawe (jina limehifadhiwa) alijeruhiwa vibaya.
Alisema
kuwa tukio hilo lilitokea saa 3:00 asubuhi eneo la Tanita wakati mtoto
huyo alipokuwa akitokea dukani akiwa ameongozana na mwenzake, mtoto wa
mama yake mkubwa mwenye umri wa miaka saba, ambaye alikuwa amewaagiza
mkate.
“Mama
yake mkubwa aliwatuma dukani Kwa Mrisho ambapo walinunua mkate na
walipokuwa wakirudi, walikutana na mtuhumiwa ambaye alimrubuni mwanangu
kuwa ameangusha chenji iliyorudi dukani hivyo aende akampe,” alisema.
Alisema
kuwa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa na pikipiki, alimchukua na kumpeleka
kwenye vichaka ambavyo viko jirani na barabara huku mwenzake akiwa
analia kuomba msaada.
“Alikwenda
naye huko vichakani na kumfanyia vitendo hivyo, mama mmoja Clara Edwin
alikuwa akipita hapo na alipomwona mtoto aliyekuwa akilia alimwuliza
imekuwaje, akamwambia mwenzangu kachukuliwa na mtu asiyemfahamu na
kuelekea eneo la tukio, ndipo mtuhumiwa alipokimbia na kuacha pikipiki
yake,” alisema.
Alisema
kuwa yeye hakuwepo nyumbani, lakini alijulishwa kuwa mwanawe kafanyiwa
mchezo huo, ambapo alipomwona mwanawe akiwa kwenye hali ile, alipoteza
fahamu.
“Majirani
walinisaidia baada ya muda nilizinduka na kumpeleka mtoto kituo cha
Polisi cha Kwa Mathias na baadaye Hospitali ya Mkoa ya Tumbi kwa ajili
ya matibabu ambapo hadi sasa anaendelea vizuri baada ya kupatiwa
matibabu,” alisema.
Kwa
upande wake, Clara ambaye ndiye aliyemuokoa mtoto huyo, alisema yeye
baada ya kwenda kule vichakani mtuhumiwa alikimbia kusikojulikana na
wasamaria waliipeleka pikipiki hiyo kwenye kijiwe anachofanyia kazi na
ndipo walipobaini kuwa ni ya Lucas.
“Wasamaria
wema wakishirikiana na madereva bodaboda wenzake, walifika nyumbani
kwao na kumkuta mlezi wake ambapo walimwambia asimruhusu kuondoka hadi
polisi watakapofika, ambapo walimchukua na kumpeleka kituoni,” alisema.
Akithibitisha
kutokea tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei
(pichani juu) alisema mtuhumiwa huyo anashikiliwa na atafikishwa
mahakamani mara upelelezi utakapokamilika