CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinatarajia kuzindua
operesheni ya kutoa elimu ya mpigakura nchi nzima, itakayoitwa Mkoa kwa
Mkoa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, John Mnyika, alisema chama hicho
kimeona Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), haijatoa elimu ya kutosha.
Alisema Chadema itaanza rasmi kutoa elimu hiyo mkoani Njombe, ambako
uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Mpigakura unatarajiwa kuanza, na
operesheni hiyo itazinduliwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman
Mbowe.
Mnyika alisema kwa kuwa Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva alitoa
hamasa kwa wanasiasa kutoa elimu hiyo, Chadema itaanza rasmi utoaji
elimu Njombe na kutaka Jeshi la Polisi kutoingilia kwa kuwa wanafanya
jambo la kikatiba.
Kuingilia uandikishaji Alipoulizwa kuhusu kutoa taarifa kwa Polisi,
Mnyika alisema walitoa taarifa kuhusu mikutano ya kutoa elimu hiyo,
lakini Polisi walijibu kuwa hiyo ni mikutano ya kisiasa na itaingilia
uzinduzi wa uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika wiki hii na mgeni rasmi
anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye yuko katika ziara ya
kikazi katika mikoa ya Iringa na Mbeya.
Hata hivyo, Mnyika alisema masuala hayo hayaingiliani na
hayahatarishi usalama wa nchi, kauli inayoonesha kuwa chama hicho
hakikubaliani na tahadhari ya Polisi.
Maandalizi tayari Uandikishaji wa wapigakura katika Daftari la Kudumu
la Mpigakura kwa kutumia mfumo mpya wa teknolojia ya kielektroniki ya
BVR (Biometric Voters Registration), unatarajiwa kuanza rasmi mkoani
Njombe kesho.
Akizungumza juzi Dar es Salaam, Jaji Lubuva alisema vifaa
vinavyohitajika mkoani humo vimeshawasili na kwa kuanza wataandikisha
wananchi wenye sifa katika mji mdogo wa Makambako.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Paulo Malala, alisema
wamejipanga vizuri na walishapata mafunzo kuanzia ngazi ya kata hadi
mkoa kutoka kwa maofisa na wataalamu wa Nec.
“Mafunzo tumepata na hata maopereta wa BVR, walishafundishwa jinsi ya
kutumia mashine hizo na kwa kweli kama wananchi watajitokeza kama
tulivyopanga, ni wazi tutamaliza kazi hiyo na muda unatosha,” alisema
Malala.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara juzi
mkoani Iringa, Pinda aliwataka Watanzania kwa ujumla wao, kujiandikisha
katika Daftari la Kudumu la Mpigakura, ili wawe na uhalali wa kuchagua
viongozi wanaowataka wakati ukifika.
“Tupo katika hatua za mwisho za kuanza uandikishaji kwa kutumia
teknolojia mpya ya kielektroniki ya BVR (Biometric Voters Registration)
na mimi mwenyewe nitafanya uzinduzi mkoani Njombe,” alisema.