Kikao cha Baraza la Madiwani la
Halmashauri ya Jiji la Tanga, kimevunjika mara tatu mfululizo kutokana
na madiwani wa Chama cha Wananchi (CUF) na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanyiana vurugu na kukunjana kutaka kuzichapa kavu kavu.
Vurugu hizo zimetokana na uongozi wa
Halmashauri ya Jiji la Tanga kuendelea kumtambua na kumwita katika vikao
vya Baraza la Madiwani wa jiji hilo aliyekuwa Diwani wa Kata ya Malungu
(CUF), Mohamed Mwambeya, wakati alishajiondoa katika chama hicho.
Mwambeya ambaye alipata udiwani wa kata
hiyo kupitia CUF, Agosti, mwaka jana, alitangaza kukihama chama hicho
na kuhamia CCM wakati wa mkutano wa Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya
Wazazi CCM, Abdallah Bulembo alipofanya ziara mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano Tanzania, nafasi zote za kuchaguliwa za kisiasa kwa maana ya
rais, ubunge na diwani, ni lazima atokane na chama cha siasa na masharti
hayo pia yapo katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Hivyo kutokana na katiba hiyo, Mwambeya
ambaye alitangaza kujiondoa CUF na kujiunga CCM ni wazi kuwa udiwani
wake utakuwa umekoma na msimamizi wa uchaguzi alistahili kutangaza kuwa
kata hiyo ipo wazi ili kufanyike mchakato wa kuchagua diwani mwingine
atakayetokana na chama cha siasa.