Mtu anayetuhumiwa kwa utapeli, amekamatwa wilayani Hanang’ mkoani Manyara akidaiwa kuwa na vyeti bandia vitatu vya ajira tofauti akidai ni mwalimu, ofisa mifugo na polisi.
Mtuhumiwa
huyo, Hamis Yusufu alikamatwa katika kata ya Gissambalang’ wilayani
Hanang kwa ushirikiano wa ofisi ya diwani pamoja na polisi jamii.
Akizungumza
na waandishi wa habari juzi, Diwani wa kata ya Gissambalang’, Masala
Bajuta, alisema mtu huyo alikamatwa Januari 10 mwaka huu saa 11 kwenye
shule ya sekondari Gissambalang’.
Alikamatwa baada ya walimu kumtilia shaka akidai anafanya mazoezi kwa vitendo shuleni hapo.
Kwa
mujibu wa diwani, mtu huyo alifika shuleni hapo na kupewa hifadhi na
mmoja wa walimu baada ya kujitambulisha kwamba amefika kufanya mazoezi
kwa vitendo. Alipotakiwa kuonesha vitambulisho na vyeti vyake, alidai
kuwa alivisahau mjini Katesh.
“Huyu
mtu Hamis Yusufu alikuwa haeleweki mara aseme yeye ni mwalimu, mara
yeye ni askari polisi wa upelelezi, mara yeye ni ofisa mifugo na
alipobanwa zaidi alidai kuwa yeye ni mwananchi wa kawaida tu,” alisema Bajuta.
Alisema
Polisi Jamii walipompekua walimkuta na vyeti vitatu vilivyopigwa mihuri
japokuwa vingine havikuwa na picha yake. Alisema kitambulisho kimoja
kilikuwa na picha ya Ofisa Mifugo, George Lwakatare ikionesha
ameajiriwa mjini Singida.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Christopher Fuime alithibitisha kukamatwa
kwa mtu huyo na kusema anashikiliwa kwenye kituo cha Polisi Katesh
wilayani Hanang’ kwa uchunguzi zaidi.