Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Saidi Mawji alisema mtoto huyo,
Yadiko Chigoda amepata jeraha kichwani na sasa anaendelea kupatiwa
matibabu na uchunguzi zaidi.
“Ni kweli tumempokea mtoto huyo akiwa na mama yake na ndugu zake
wengine waliomsindikiza, ameumia sana kichwani lakini bado anaendelea na
tiba na uchunguzi zaidi kwenye fuvu la kichwa maana inaonesha kama
limepasuka,” alisema.
Pia, Dk Mawji alisema wanafanya mpango wa kumhamishia mtoto huyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu zaidi.
Akizungumza katika wodi namba saba katika hospitali hiyo, mama mzazi
wa mtoto huyo, Caroline Mnyawami (32) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha
Mingui Kata ya Lumuma, alisema siku ya tukio majira ya saa nne mume
wake, Fabian Chigoda alikuwa akimpiga kaka yake na ndipo akajaribu
kuamulia ugomvi huo.
Alidai alipojaribu kumnyang’anya mumewe fimbo, aliyokuwa akimpigia
kaka yake, ndipo mumewe aliamua kuchukua mchi wa kinu na kumrushia
kichwani, ambapo alikwepa na kisha mchi huo kumgonga mtoto, aliyekuwa
amembeba mgongoni.
Baada ya mwanaume huyo kuona amempiga mtoto, aliamua kukimbia na
mpaka sasa hajulikani alipo. Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mingui,
Mwingwa Udoba, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema chanzo cha
ugomvi ni masuala ya kifamilia.
“Bado tunaendelea kumtafuta, kwani alikimbia baada ya tukio na akipatikana atafikishwa kwenye mikono ya sheria,” alisema.