Watu wawili wamefariki dunia baada ya kimbunga kupiga katika Kisiwa cha Goziba na kusababisha baadhi ya mitumbwi kupinduka katika Ziwa Victoria.
Kimbunga hicho kilitokea juzi saa tano asubuhi wakati wakazi mbalimbali wakiwa katika shughuli zao.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Rembris Kipuyo alisema jana kuwa, majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.
Alisema kimbunga hicho hakikuwa cha kawaida kwa kuwa kiliharibu nyumba na zaidi ya mitumbwi arobaini imepotea.
Miongoni
mwa walionusurika, Mariagoreth Phares alisema tukio hilo lilikuwa kama
muujiza kwa kuwa aliona kitu kilichosogea kutoka angani.
Alisema nyumba zilianza kung’olewa kwa upepo na watu kurushwa majini, huku wengine wakipoteza fahamu.
Alisema
baadhi ya watu walikuwa wakijaribu kujiokoa kwa kutambaa ili wasipigwe
na vitu vilivyokuwa viking’olewa na kurushwa na upepo.
Majeruhi mwingine Leah Lazaro alisema aliona kitu kilichokuwa kinachemsha maji kwa kasi ziwani kuelekea kwenye kisiwa hicho.
“Nilikuwa
mwaloni nikaona kitu kinachemsha maji kwa kasi nilikimbia na
kumkumbatia mtoto wangu ambaye aliniponyoka,” alisema Lazaro.
Kisiwa cha Goziba kipo umbali wa kilomita 80 kutoka Wilaya ya Muleba na kipo karibu zaidi na Mkoa wa Mwanza.
Wakazi
wa kisiwa hicho hupata mahitaji yao Mwanza. Kipuyo alisema baada ya
kamati ya maafa kutembelea eneo hilo, itatoa tathimini ya kiwango cha
hasara kilichotokea.
Aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia wakazi wa kisiwa hicho ambao wengi wao wamepoteza mali.