Jumuiya ya Vijana ya CUF (JUVICUF) imemtaka Waziri wa Mambo ya
Ndani, Mathias Chikawe kufuta kesi zote zilizofungliwa kutokana na tukio
lililotokea mapema wiki hii la viongozi wa chama hicho na wafuasi
kupigwa na kukamatwa na polisi.
Jumuiya hiyo, pia
imesema kuwa itaandaa maandamano nchi nzima kulaani vitendo vya
ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyofanywa na askari wa Jeshi la Polisi
vya kuwapiga wafuasi wa vyama vya upinzani na kuwafungulia mashtaka.
Wakati
jumuiya hiyo ikitoa tamko hilo, kituo cha Haki za Binadamu kimelaani
vikali kitendo cha polisi kupiga viongozi hao na wafuasi wa CUF,
kikisema kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba Jeshi la Polisi
linaonyesha upendeleo kwa chama tawala CCM ambacho kinaruhusiwa kufanya
mikutano yake wakati wapinzani wanawekewa mizengwe.
Akizungumza
kwenye mkutano na waandishi wa habari jana, mwenyekiti wa JUVICUF,
Hamidu Bobali alisema kabla ya kufanya maandamano hayo, wanamtaka Waziri
Chikawe ajiuzulu na Serikali ifute kesi zote zinazotokana na tukio
hilo.
“Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Ernest Mangu
asikubali kuliacha jeshi hilo lionekane ni la watu waliokosa nguvu ya
kujenga hoja mbele ya umma. Hoja ya kuibiwa silaha kutoka Kituo cha
Polisi cha Ikwiriri haikuwa na uhusiano na maandamano ya CUF, hivyo ni
vema akakanusha hoja hiyo na tunaiita ya kitoto na isiyo na mashiko,
“alisema Bobali.
Profesa Lipumba na wafuasi 30 wa CUF
wamefunguliwa mashtaka ya kula njama, kukukusanyika na kuandamana bila
ya kibali na tayari kiongozi huyo alipata dhamana juzi, huku wafuasi hao
wakipata dhamana jana.
Mapema wiki hii, viongozi na
wafuasi wa CUF walipigwa na kukamatwa na polisi kwa madai ya kuandamana
bila kibali wakati wakiadhimisha mauaji ya wenzao waliouawa na polisi
mwaka 2001. Wafuasi hao walikuwa wakiandamana kupinga matokeo ya
uchaguzi wa Rais wa Zanzibar mwaka 2000.
Katika machafuko hayo, watu kadhaa wa kisiwani Unguja walikimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya kuepuka vurugu hizo.
Katika machafuko hayo, watu kadhaa wa kisiwani Unguja walikimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya kuepuka vurugu hizo.
Kuhusu maandamano, Bobali alisema
pamoja na kupigwa, jumuiya hiyo inaandaa maandamano mengine kulaani
vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyofanywa na Jeshi la
Polisi.
Bobali alisema wameazimia kuandaa maandamano
nchi nzima kupinga vitendo alivyoviita vya kinyama baada ya viongozi wao
kwa kupigwa eneo la Mtoni Mtongani.
Alisema
kilichofanyika ni unyama na uhuni kwa sababu suala la wao kuandamana kwa
ajili ya kuwakumbuka wanachama wenzao hufanyika kila mwaka na huu ni
mwaka wa 13 haijawahi kutokea kama walivyofanyiwa mwaka huu.
Katika
hatua nyingine, mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho cha haki za
binadamu, Helen Kijo-Bisimba alisema kitendo cha kuwafyatulia mabomu ya
machozi na kuwajeruhi wananchi waliotii amri ya kutawanyika, ni uvunjaji
wa haki za binadamu unaofanywa na polisi.
Alisema
Polisi wanapaswa kujitathmini upya kwa sababu CCM imekuwa ikiruhusiwa
kufanya mikutano wakati vyama vya upinzani vinawekewa mizengwe kuwa
mikutano yao inaweza kutumiwa na magaidi.
“Polisi
wanasema mikutano ya vyama vya upinzani inaweza kusababisha matukio ya
kigaidi, mbona CCM inaendelea na mikutano. Je, matukio ya kigaidi
hayawezi kutokea kwenye mikutano ya chama tawala,” alihoji Bisimba
katika taarifa yake.
Bisimba alisema kituo hicho
kinalaani sababu za kiintelijensia zisizotajwa ambazo zimekuwa
zikitumiwa na polisi kuzuia mikutano ya vyama vya upinzani.
“Kituo
kinaitaka Polisi kuhakikisha kuwa wanazielewa na kuzitii sheria
zinazowaongoza katika kazi zao kwani kwa kufanya hivyo wataepusha
matumizi ya nguvu dhidi ya raia ambayo husababisha majeruhi na maafa."
Wakati
huohuo, wafuasi 30 wa CUF wanaokabiliwa na mashtaka ya kula njama na
kukaidi amri halali ya polisi na kufanya maandamano, wameachiwa baada ya
kukamilisha masharti ya dhamana.
Hakimu Mkazi wa
Mahakama ya Kisutu, Emillius Mchauru jana aliwaachia huru washtakiwa hao
baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kila mshtakiwa kuwa na
mdhamini mmoja anayeaminika na kila mdhamini asaini hati ya dhamana ya
maneno ya Sh100,000.
Baada ya washtakwia hao
kukamilisha masharti hayo ya dhamana, Hakimu aliiahirisha kesi hiyo hadi
Februari 12 kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika.
Sakata
la kupigwa kwa wafuasi hao lilisababisha kikao cha Bunge cha Jumatano
kuvurugika baada ya mbunge wa kuteuliwa na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi,
James Mbatia kutaka chombo hicho kisitishe shughuli zake kwa ajili ya
kujadili jambo la “dharura kwa maslahi mapana ya Taifa”.
Lakini
Spika Anne Makinda alisema suala hilo lingejadiliwa siku inayofuata,
maelezo ambayo yalipingwa na wabunge, hasa kutoka vyama vya upinzani,
ambao waliamua kusimama na kupiga kelele na kusababisha Spika ashindwe
kuendelea na kikao hicho na hivyo kuahirisha hadi Jumatano.
Katika
kikao cha Jumatano, ulizuka utata wa mgongano wa mihimili mitatu ya
nchi baada ya Mwanasheria Mkuu, George Masaju kuwataka wabunge
wasijadili suala hilo kwa kuwa ni kuingilia mahakama, lakini Spika
akaruhusu mjadala huo, ambao ulitawaliwa na shutuma nyingi dhidi ya
Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri Chikawe.