Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kurukekere katika Wilaya ya Bunda wanafanyishwa kazi za vibarua mashambani na walimu ili kupata fedha za kununulia chaki za kufundishia kitendo ambacho kimelalamikiwa vikali na wananchi.
Wakitoa malalamiko yao wananchi hao walisema wanafunzi wamekua wakitumia muda mwingi kufanya kazi za vibarua zikiwemo za kulima mashamba ya watu binafsi wakati wa vipindi vya masomo ikiwa ni pamoja na kutembea umbali mrefu kwenda kwenye mashamba hayo.
Walisema baada ya kuona watoto wakiwa kwenye mashamba hayo walikwenda kuwahoji walimu wao na walijibiwa kwamba wanafanya hivyo ili zipatikane fedha za kununulia chaki na mahitaji mengine ya shule hiyo.
Aidha walisema hali hiyo imewafanya wanafunzi kukosa muda wa kusoma na kuchangia kusuka kwa kiwango cha ufaulu kwa kiasi kikubwa tofauti na miaka ya nyuma.