WANAUME wanne wataishi gerezani miaka 40 kila mmoja kwa
kumuua mwanajiolojia Campbell Rodney Bridges wa Uingereza miaka mitano
iliyopita.
Jaji Maureen Odero wa Mahakama Kuu
ya Mombasa, aliwapa adhabu hiyo Mohamed Dadi Kokane mwenye umri wa miaka
42, Alfred Njuruka Makoko (58), Samwel Mwachala Mwaghania (49) na James
Chacha Mwita wa miaka 56 siku moja baada ya kuwapata na hatia ya kumuua
Bridges.
Jaji Odero alisema kwenye hukumu
yake kwamba kosa walilotenda ni mbaya na walikatiza maisha ya marehemu
aliyeacha mjane na mtoto mvulana.
Ingawa upande wa mashtaka uliomba
mahakama iwahukumu kunyongwa, jaji alisema kuna tashwishi kuhusu ikiwa
adhabu hiyo ni ya lazima kwa sababu ya maamuzi mawili tofauti ya
mahakama ya rufaa.
Kabla ya kuhukumiwa, kiongozi wa
mashtaka George Muriithi alisema walitenda kosa mbaya ambalo walipanga.
“Hakuna kinachoweza kuzuia adhabu katika kesi hii, lazima wanyongwe”.
Kulingana na ripoti ya waathiriwa wa
mauaji iliyowasilishwa kortini, mjane wa marehemu Judith Bridges
alisema uchungu wa kumpoteza mumewe uliathiri familia yake.
Kwenye malilio yao, washtakiwa
kupitia mawakili Steve Kithi na Fredrick Mwawasi, walisema wana familia
na wakaomba wapewe adhabu nafuu.
Aidha, waliomba korti itilie maanani muda ambao baadhi yao wamekuwa rumande na walipoachiliwa kwa dhamana kesi ikiendelea.
Jaji Odero alisema kwamba walikuwa miongoni mwa kundi la watu waliomshambulia Bridges akielekea katika kambi yake.
“Nimeridhika upande wa mashtaka
umethibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa wa kwanza, pili, tatu, nne na
kundi lao kwa kutekeleza nia ya kutenda uhalifu waliopanga,” akasema.
Jaji Odero aliongeza kuwa washtakiwa walivunja sheria kwa kufunga barabara na kumzuia marehemu asifike kambi yake.
“Washtakiwa wanawajibika kwa kupotea
kwa maisha ya marehemu. Walimvamia na kundi lake licha ya kuwa hakuwa
na silaha, hakuwawatisha,” akasema.
Marehemu aliuawa mnamo Agosti 11,
2009 katika eneo la Kambaga Mwasui, Mwatate, Kaunti ya Taita Taveta.
Alikuwa mwanajiolojia aliyehusika na uchimbaji nchini tangu 1974 na
alikuwa na kampuni mbili.
Jaji alisema kwamba mashahidi
walithibitisha kulikuwa na mzozo wa muda mrefu kati ya marehemu na kundi
la 'wachimbaji eneo hilo’ kuhusu maeneo ya kuchimba madini ya Mwasui na
Mkuki.
Ushahidi wa kutosha
“Mzozo huu ulipelekea kifo cha
ghafla cha marehemu alasiri ya Agosti 11 2009,” akasema Jaji Odero na
kuongeza kuwa waliomshambuliwa walifahamika na mashahidi.
“Walikutana kila mara na wote
walihusika na uchimbaji madini, kwa hakika mashahidi walimtambua kila
mmoja kwa jina lake,” akasema.
Jaji Odero alisema utetezi wa Kokane haukufaa, ilhali wa Makoko hakuweza kumshawishi.
Alisema Mwachala alitambuliwa vyema
na mashahidi wote kama mmoja wa waliomshambulia marehemu ilhali utetezi
wa Mwita haukuwa na chochote cha kutiliwa maanani.
Hata hivyo, aliwaachilia Daniel
Mdachi Mnene, Osman Abdi Hussein na Crispus Mkunguzi Mngolia
walioshtakiwa kwa kuhusika na mauaji ya Bridges.
Jaji alisema kulikuwa na shaka ikiwa
Mnene na Mkunguzi walihusika na shambulio dhidi ya marehemu, na
akamwachilia huru. Alisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya
Hussein.
Upande wa mashtaka uliwaita mashahidi 26 katika kesi hiyo akiwemo mke wa marehemu na mwanawe.
