JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu
wawili wanaotuhumiwa kufanya vitendo vya utekaji, unyanyasaji wa
kijinsia na mauaji ya wanawake.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman Kova alisema hayo jana
jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema watuhumiwa hao wamehusishwa na vitendo hivyo baada ya
upelelezi wa kina na wa kitaalamu uliosaidia kuwakamata wahalifu hao
wakiwa na vielelezo mbalimbali.
Kova aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni wakazi wa Dar es Salaam,
Abubakar Amani (28) wa Mwenge katika Manispaa ya Kinondoni na Ezekiel
Kasenegala (25) wa Tandika, katika Manispaa ya Temeke.
Pia alisema watuhumiwa hao walikiri kuhusika na mauaji ya Wenze
Makongoro (23), aliyekuwa mwanafunzi wa Stashahada ya Ukutubi katika
Chuo cha Bagamoyo na Jacqueline Frederick (30), mkazi wa Kisarawe.
‘’Watu hao waligundulika kuuawa Novemba 19 mwaka huu na kutupwa maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam,’’ alisema Kova.
Aliongeza kuwa baada ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao walikutwa na
vielelezo mbalimbali zikiwamo suruali mbili za kike, sketi moja, kikoi
kimoja, mikoba minne ya kike na simu moja aina ya Tecno.
Pia walikutwa na sidiria moja, vidani vya mikononi viwili, pete moja,
hereni jozi tatu, vibanio vya nywele, vipodozi vya kike na shanga tatu.
Alisema katika mahojiano na watuhumiwa hao walijihusisha na ulaghai
wa kimapenzi, utekaji nyara, kuwawekea dawa katika vinywaji watu hao na
kuwanyanyasa kijinsia na kusababisha mauaji.
Alitoa onyo kwa wanawake hasa wasichana na wanafunzi wa kike
kutokukubali kuingia katika mahusiano ya kimapenzi haraka na watu
wasiowafahamu.
Alisema watuhumiwa hao wata- fikishwa mahakamani muda wowote kwani upelelezi umeshakamilika