Hakika teknolojia inazua mengi, hata yale ambayo hayakuwahi kufikiriwa na mababu zetu karne nyingi zilizopita.
Hivi karibuni, wanasayansi wameweza kugundua namna
ya kuzisafisha mbegu za kiume za mtu mwenye virusi vya Ukimwi na
kuondoa virusi hivyo ili kumwezesha kutungisha mimba bila kumwathiri
mwenza wake.,
Hii ni kwa wenza ambao mwanamume anaishi na VVU na mwanamke akiwa hana virusi hivyo.
Programu hiyo maalumu ijulikanayo kama SPAR,
ilibuniwa ili kuwasaidia wenza hao kupata mtoto bila kumwambukiza mama
na mtoto ambao mwanamume anaishi na VVU aweze kuzalisha.
Inafanyikaje?
Kisayansi, damu pekee si kipimo cha kuonyesha kuwepo kwa maambukizo ya VVU katika mwili bali hata katika majimaji ya mwilini.
Ogani zinazozalisha majimaji ya mbegu za kiume huathiriwa kwa namna ya pekee na VVU.
Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa magonjwa, Henry
Mwakyoma anasema kwa kawaida Virusi vya Ukimwi hupenda kukaa katika
chembehai nyeupe(CD4).
“Kwa kawaida VVU haviishi katika mbegu za kiume.
Lakini hupendelea zaidi kukaa katika CD4 au chembehai nyeupe za damu
ambazo zipo katika damu na katika majimaji ya mbegu za kiume au semen,”
anasema.
Anasema ndiyo maana inawezekana mwanamume mwenye VVU asimwambukize mwenza wake.
“Kama hana michubuko mwanamke anaweza asipate
maambukizo, kwa kuwa majimaji ya mbegu za kiume yanakosa mahali pa
kuingia,” anasema.
Hata hivyo, Dk Mwakyoma aliona kuna ugumu
kuzisafisha mbegu za kiume na kuondoa majimaji yake yenye VVU, ili
kuzipandikiza mbegu hizo ili zitungishe mimba kama unavyosema utafiti
huo.
