Rais Jakaya Kikwete ameongeza miezi sita ya kukamilisha ujenzi
wa maabara katika shule za sekondari nchini, baada ya muda wa miaka
miwili alioutoa awali kumalizika Novemba 30, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Ikulu jana, ilieleza kuwa Rais Kikwete amechukua uamuzi huo ili
kuwezesha kazi hiyo inayoendelea nchini kote kufanyika kwa usahihi.
Ikulu ilieleza kuwa Rais Kikwete alitoa maelezo
hayo Desemba 18, 2014, baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu
na Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyopo
Arusha, Dk Mohamed Gharib Bilal ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Ikulu, kiongozi huyo wa nchi
alitumia nafasi hiyo kutangaza kwamba atachangia Sh200 milioni katika
Mfuko Maalumu wa Dhamana wa taasisi hiyo ya pekee nchini.
Akizungumzia ujenzi wa maabara alisema: “Natoa
pongezi za dhati kwa viongozi na wananchi wa Tanzania kwa kazi kubwa na
nzuri waliyofanya. Kwa ajili ya kumaliza palipoishia, nawaongezea miezi
sita.”
Rais Kikwete alisema tathmini inaonyesha kuwa
shule 3,463 zinahitaji maabara, zikiwa sawa na vyumba 10,389, lakini
hadi Desemba 7, 2014, vilikuwa vimejengwa vyumba 3,867 sawa na asilimia
37.2 ya mahitaji ya vyumba vilivyokamilika.
Aliongeza kuwa vyumba 5,891, sawa na asilimia 56.7
viko katika hatua mbalimbali za kukamilishwa, huku 631 sawa na asilimia
6.1 ujenzi wake haujaanza.
Alieleza kuwa umuhimu wa kujenga maabara
uliongezwa kasi na ongezeko kubwa la shule za sekondari, ambazo
zimeongezeka kutoka shule 828 mwaka 2004, hadi kufikia 3, 551 kwa sasa.
Hata hivyo, kati ya shule hizo 3,551 ni shule 88
ndizo zilizokuwa na vyumba vitatu kwa ajili ya masomo ya fikizia, kemia
na biolojia.
Novemba 2012 Rais Kikwete alitoa muda wa miaka
miwili hadi Novemba 30 mwaka huu kukamilisha ujenzi wa maabara katika
sekondari nchini nzima.
Hata hivyo, hadi muda unamalizika, maeneo mbalimbali yalikuwa hayajatimiza agizo hilo.
