IDADI YA WATUHUMIWA WA MAUAJI YA KITETO YAZIDI KUONGEZEKA

Watuhumiwa wengine watatu wamefikishwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, wakituhumiwa kwa mauaji ya wakulima saba yaliyotokea kwenye kata za Matui na kufikisha idadi ya watuhumiwa 16.
 
Awali, kulikuwa na watuhumiwa 13 waliofikishwa mahakamani hapo ila juzi waliongezwa watatu kwenye kesi hiyo ambao ni Leitinga Simon (26) na Lekomoi Pati (20) wote wakazi wa Kijiji cha Ngeroni na Popo Lemnae (23) mkazi wa Matui.
Ilidaiwa mahakamani hapo mjini Kibaya na mwendesha mashtaka Mbaruku Mohamed, mbele ya hakimu Majidi Hudi, kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo kati ya Novemba 11 na 12, mwaka huu.
Hata hivyo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwenye mashtaka hayo kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo na Hakimu Hudi aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 30 itakapotajwa tena.
Kwenye kesi hiyo watu wanne kati yao wameshtakiwa kwa mauaji pekee na watu tisa wameshtakiwa kwa mauaji hayo na pia kudaiwa kuiba mifugo ambayo ni ng’ombe 309 zenye thamani ya Sh213 milioni mali za wafugaji wa Kijiji cha Matui.
Mohamed aliwataja washtakiwa hao wanne waliohusika na mauaji kuwa ni Kirundi Sisini (45), Lazaro Pastei (30) na Yokoyeti Koroboi (20) wote wakazi wa Kijiji cha Ilela na Kimai Enongoi (35) mkazi wa Kijiji cha Namelock, wilayani Kiteto.
Aliwataja walio na kesi ya mauaji na kuiba mifugo 309 ni Seif Juma (40), Mohamed Ahamad (18), Shaabani Mkoloni (21), Said Hatibu (29), Nasoro Hassan (25), Ayub Musa (18) Lucy Yohana (30) Abasi Mohamed (25) wote wakazi wa Dosidosi na Mashaka Chibaleu (27) mkazi wa Kijiji cha Engusero.
Alisema washtakiwa hao wanadaiwa kuwaua Hassan Kundajo (62), Salum Iddi Juma (70) Lematui Sendalo (46), Julius Andrew(50), John Makavu (42), Juma Omari Bakari (65) na Maria Ole Siriana (36).


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo