KOCHA
wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo amewaaga rasmi leo asubuhi wachezaji wa
timu hiyo kwenye mazoezi uwanja wa Sekondari ya Loyola huku akitarajia
kuvuna zaidi ya Milioni 20 ndani ya klabu hiyo ikiwa ni mshahara wake wa
dola 1200 na yupo kwenye harakati za kudai fidia ya kuvunjiwa mkataba
na kuletwa mrithi wake kabla uongozi wa klabu hiyo haujamaliza nae.
Hata
hivyo, tayari Maximo ameaga wachezaji wake kwenye mazoezi ya asubuhi leo
ambapo mazoezi hayo yaligeuka shubiri baada ya Maximo kuwakusanya
wachezaji wake na kuwambia kuwa kuanzia leo sio kocha wa timu hiyo tena
na kuwatakia maisha mema ndani ya klabu hiyo ya Jangwani.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti wachezaji wa klabu hiyo ambao pia hawajaridhishwa
na uamuzi wa uongozi wa klabu hiyo kumuacha mshambuliaji Hamis Kiiza na
kumsajili Amis Tambwe.
Mmoja wa wachezaji hao alisema "Ni kweli kocha ametuaga asubuhi daa! ndio hivyo tumesikitika lakini hatuna jinsi."
Naye
mchezaji mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema "Inaumiza
sana jana (juzi) tumefanya nae mazoezi vizuri kabisa tena amechangamka
kama kawaida kumbe nyuma kuna mambo yanaendelea, leo asubuhi tumeenda
mazoezi kama kawaida tukijua tunafanya mazoezi matokeo yake anasema
acheni kila kitu kaeni hapo nataka kuzungumza na nyinyi.
"Uwezi
kuamini kidogo machozi yanitoke pale aliposema kuanzia leo yeye sio
kocha wetu tena, dah inaumiza sana, mtu ambaye mmemzoea mnafanya nae
kazi kuondoka, ndo hivyo wakubwa wemeshaamua bwana wenye timu yao.
Wakati
huyo akisema hayo, mchezaji nguli wa timu hiyo yeye alisema "Hakuna
mchezaji kwa kweli aliyependezwa na kitendo cha uongozi, yani kwenye
mazoezi asubuhi ilikuwa kama msiba, 'mood' ya kufanya mazoezi iilisha
kabisa, yani hakuna aliyekuwa na hamu ya kuendelea na mazoezi.
"Tumefanya
kidogo mazoezi tukaondoka, ukiangalia ni sawa tumefungwa cha muhimu
ilikuwa ni kukaa chini na kuzungumza na kuangalia cha kufanya, kama kuna
mapungufu basi yafanyiwe kazi, mimi sijaona haja ya kumfukuza kocha
hasa kipindi kama hichi."
Meneja
wa timu hiyo Hafidhi Saleh alikiri Maximo kuaga wachezaji kabla ya
mazoezi ya timu hiyo kuanza akiwapa moyo wajitume kwa kuwa ni wachezaji
wazuri na timu ni nzuri na kuwataka kuongeza bidii ili wafike mbali.
"Kwa
kweli inasikitisha hakuna mchezaji wala mtu aliyefurahia, kama yupo
labda kimoyomoyo ila dah imetuumiza, ni mazoea cha muhimu tugange yajayo
hayo mengine tuwaachie viongozi."alisema Saleh
Saleh
alisema kuwa tayari kocha Hans van Der Pluijm ambaye amefikia kwenye
hoteli ya Tansoma jana alikuwa kwenye mazungumzo na uongozi wa klabu
hiyo ili aichukue nafasi ya mbrazil Marcio Maximo ambaye amekumbwa na
kipunga cha kutimuliwa baada ya kunyukwa mabao 2-0 katika mechi ya mtani
Jembe, akiwa ni kocha wa pili kutimuliwa Yanga baada ya matokeo ya
mtani jembe mwaka jana alitimuliwa Ernie Brandts baada ya kunyukwa mabao
3-1 na nafasi yake kuchukuliwa na Pluijim ambaye nae hakukaa sana
akaikacha timu hiyo baada ya kupata kibara nchini Saudi Arabia.
Wakati
huo huo, uongozi wa Yanga umegwaya mchezaji Andry Countinouh kuvunja
mkataba wake baada ya kuwa wangelazimika kuvunja kibubu cha Sh185
milioni ili kumlipa fidia ya mshahara wake ambao ni dola 2800 kwa mwezi.
Katika
hatua nyingine, pamoja na Yanga kumfungashia virago Emerson De Oliveira
Neves Roque imemuombea kibali cha usajili wa kimataifa (ITC) kutoka
Bonsucesso Brasil kwenda Yanga.
Mkurugenzi wa mashindano ya TFF, Boniface Wambura alisema kuwa TFF haina taarifa za Yanga kumuacha mbrazili huyo.
