Claudia Kayombo
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp
Kardinali Pengo, amefichua siri ya kupona maradhi yaliyokuwa
yakimsumbua kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Alisema alikaa chini ya msalaba wa Yesu Kristo akimwomba naye alifanyia huruma kwa kumponya.
Pia, aliwashukuru maaskofu wasaidizi wake, Eusebius Nzigilwa na Titus Mdoe kwa kufanya kazi vizuri wakati akiwa katika matibabu.
Mwadhama Pengo alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam, wakati akitoa
neno la shukrani baada ya Ibada ya Misa takatifu aliyoadhimisha kwenye
Kanisa Kuu la Kiaskofu la Mtakatifu Yosefu, ambalo ni makao makuu ya
jimbo hilo.
Pamoja na mambo mengine, ibada hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kutimiza miaka 70, tangu alivyozaliwa.
“Katika kipindi hicho, namshukuru Mungu kwa kuwa amenionesha mapendo,
kama Yohana yule mwanafunzi ambaye alipendwa na Yesu na alisimama chini
ya msalaba wake naye akamkabidhi mama yake Bikira Maria.
“Pamoja na mambo mengine, kwa namna ya pekee niliposimama chini ya
msalaba alinikabidhi mama yake, nilikuwa mtoto katika familia yake. Kwa
nini niseme mimi kama Yohana yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu
kutokana na mambo makuu haya aliyonitendea,” alisema.
Alibainisha kuwa, alikuwa amekabiliwa na changamoto za maradhi ambayo
hata hivyo, hakuyataja, katika kipindi cha mwaka mmoja lakini wasaidizi
wake walifanya kazi kwa busara na hekima ya hali ya juu bila hata yeye
kuwaelekeza lolote.
“Kutokuwepo kwangu katika kipindi cha mwaka mmoja, jimbo
halikuteteleka, pamoja na sala zenu asante sana kwa moyo wenu wa
kujitoa.
“Kwa kadri Mwenyezi Mungu atakavyonipa nguvu na uwezo wa kufanya kazi
katika kipindi changu cha ujana wa miaka 70, nitaendelea kuwatumikia,
kwa njia ya sala na maombi nitakuwa pamoja nanyi kwa nguvu zaidi,
Mwenyezi Mungu atujalie sote miaka mingi kwa kadiri ya mpango wake.
“Kabla Mungu hajanichukua ningependa Jimbo la Dar es Salaam liwe limetimiza parokia 100,” alisema.
Aidha, Mwadhama Pengo aliwashukuru mapadri wote na watawa wa jimbo
hilo kuwa, walionesha ushirikiano mzuri na wasaidizi wake na hivyo jimbo
hilo kuendelea vizuri.
Hata hivyo, baada ya kumaliza ibada hiyo ya misa takatifu kulifanyika
hafla fupi ya kumpongeza iliyohudhuriwa na wasaidizi wake, mapadri,
watawa wa kiume kwa wake pamoja na wawakilishi kutoka jumuia mbalimbali
katika jimbo hilo.
Awali, Askofu Msaidizi Mdoe katika mahubiri yake, alisema Mwadhama
Pengo aliyetimiza miaka 70 Agosti 5, mwaka huu, siku hiyo alikuwa nchini
India katika matibabu.
Alisema katika nchi hiyo, alikwenda zaidi ya mara ya tatu kupata matibabu na huko Ujerumani nako mara moja.
Hata hivyo, alisema kwa neema ya Mungu anaendelea vizuri huku
akifurahia miaka 43 ya upadri, 30 ya uaskofu na miaka 16 ya uaskofu
mkuu.
Aidha, Mdoe alisema katika kipindi hicho aliitumia vema talanta
aliyopewa na Mungu kwa kufanya mambo mazuri ya mfano nchini na hata nchi
za nje.