VYOMBO vya habari nchini vimeaswa kuripoti matukio yaliyofanyiwa uchunguzi wa kina na yenye kufuata maadili na taaluma ya habari, badala ya kufanya kazi kwa kuongozwa na ushabiki vinapotekeleza majukumu yake.
Hayo
yameelezwa katika taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu
iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari ikikanusha kuhusika kwa Katibu wa
Rais Jakaya Kikwete, Prosper Mbena katika kumpa mwongozo Gavana wa
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu ili auruhusu uchotwaji
wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyopo katika BoT.
Taarifa
hiyo inasema baadhi ya vyombo vya habari (Siyo EDDY BLOG) vimemhusisha
Mbena kuingilia mchakato wa uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 306 katika
akaunti hiyo iliyoibua hoja nzito nchini, kiasi cha Bunge kuingilia kati
na kutaka baadhi ya mawaziri na watendaji serikalini wawajibike kwa
kile kinachodaiwa kuchota fedha za umma, jambo ambalo bado
halijathibitishwa rasmi. “Huu ni uongo na uzushi."
Ni jaribio jingine la kutia chumvi katika jambo ambalo limetawaliwa kwa kiasi kikubwa na mihemko ya aina yake.
Gavana
Ndulu mwenyewe anathibitisha kuwa hajawahi kupokea barua yoyote kutoka
kwa Katibu wa Rais kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow.
Akaunti ya Escrow ilifunguliwa baada ya kutokea kwa mgogoro wa kimaslahi baina ya kampuni ya kufua umeme ya IPTL na Tanesco.