Mnamo tarehe 4 Desemba 2014, Gazeti la Raia Tanzania, Toleo Na.0259 liliandika habari iliyokuwa na kichwa cha habari “Waziri Muhongo ‘atimkia’ Norway”.
Gazeti
hilo lilieleza kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo ambaye anapaswa kuwajibishwa kwa mujibu wa ushauri wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano, yuko kikazi nchini Norway ambako ameongozana na
viongozi waandamizi wa Wizara yake.
Wizara
inatoa taarifa kwa Watanzania kwamba habari hiyo haina ukweli wowote
kwani Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo yupo hapa
nchini na tarehe ambayo gazeti husika lilichapisha habari hiyo, Mhe.
Muhongo alikuwa wilayani Musoma, mkoani Mara kuhudhuria hafla ya
kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri kwenye masomo katika shule ya
Msingi ya Mwisenge A na B.
Waziri
Muhongo alihudhuria hafla hiyo baada ya kualikwa na Ubalozi wa China
hapa nchini, ambao umetoa ufadhili wa masomo na zawadi kwa wanafunzi
walemavu wapatao 108 waliofanya vizuri katika masomo yao. Aidha, Ubalozi
wa China umetoa ufadhili wa kuwapeleka baadhi ya wanafunzi kutoka
katika shule hizo kwenda nchini China kwa lengo la kujifunza utamaduni
wa nchi hiyo.
Ufadhili
huo wa masomo umetolewa na Ubalozi wa China kwa ajili ya kumuenzi Baba
wa Taifa Mwl. Julius. K. Nyerere ambaye alisoma katika shule hiyo.
Hafla
hiyo pia ilihudhuriwa na Balozi Mdogo wa Ubalozi wa China Bw. Li
Xuhang, Meya wa Mji wa Musoma Mhe. Alex Kisulura, Mhe. Madaraka Nyerere,
Bw. Joseph Kahama pamoja na walimu na wanafunzi wa shule hizo.
Tunapenda
kuwakumbusha waandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma na
uzalendo ikiwa ni pamoja na kuandika habari zilizofanyiwa uhakiki na
zenye ukweli, zisipotoshe Umma ili kuondoa usumbufu kwa wananchi.
Imetolewa na,
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
5 Desemba 2014