HAKUNA kitu kinachowasumbua wengi katika uhusiano kama kutokuwa na
uhakika na hisia za mwenza wako kwako. Wengi wamekuwa wakijaribu kwa
hali na mali kutaka kujua kama kweli mwenza aliye naye anampenda au yuko
naye kwa ajili ya tamaa na endapo akimaliza shida zake huenda
ukamuacha.
Zipo njia nyingi unazoweza kuziangalia na kujua kama kweli mwenza
uliye naye ana nia na upendo wa kweli kwako, njia hizo ni pamoja na
kuangalia mienendo yake anapokua na wewe au mbali nawe.
Ukitaka kujua kama mwenza wako anakupenda na kukujali, lazima awe na
kumbukumbu ya kile ulichokisema, hapa hasa kwa wanaume, hata kama mwenza
wake amesema jambo lisilo na maana lakini kwa kuwa anampenda na kumjali
hujitahidi kuwa makini na kumsikiliza na hivyo kuwa na kumbukumbu
nzuri.
Aidha ili kujua kama mwenza wako ana hisia nzuri kwako, utaona namna
anavyokuchukulia mkiwa pamoja, hujaribu kufanya yale yanayokupendeza na
kamwe hatokubali uumie au upate taabu.
Jambo lingine ni pale anapokushirikisha katika mipango yake ya
maisha, endapo mwenza wako atazungumzia ndoto zake za maisha ya baadaye
bila kukuhusisha ujue kuwa uhusiano huo hauna hisia za upendo.
Mwenza anayekupenda katika mipango lazima akushirikishe ikiwa ni
pamoja na kukujumuisha katika mipango hiyo.
Aidha unaweza kutambua kama
unapendwa au la na mwenza wako, pale mnapokua kwenye umati wa watu wengi
wakiwemo rafiki zake, anapokua jirani na wewe, kukushika mkono na
kutoona aibu ya kukutambulisha, ukiona hivyo tambua wazi kuwa hisia za
mwenza wako kwako ni za kweli.
Dalili nyingine ni pale mwenza wako anapoanza kufuatilia nyendo zako
na kuonesha wivu wa waziwazi kwako, kutokupendezwa pale anapokuona
unazungumza kwa ukaribu na wanaume au wanawake wengine tofauti na wewe.
Wenza wengine wanaonesha upendo wao kwa kuhakikisha anajua kila kitu
kuhusu maisha yako na kuwa tayari kusaidia pale panapoonekana panahitaji
msaada na endapo mnagombana huwa tayari kumaliza ugomvi kwa njia nzuri
ya maelewano na si kuwekeana visasi.
Aidha jambo lingine ni pale unapoona anajitahidi kwa hali na mali
kufahamiana na ndugu zako lakini kikubwa akijitahidi sana ndugu zako hao
wamkubali.
Ukweli ni kwamba zipo dalili nyingi zinazoweza kukusaidia kutambua
kuwa uhusiano ulionao ni wa kudumu au la, jambo la msingi ni kuhakikisha
kuwa hata wewe mwenyewe unajitahidi kuwa chachu ya kuimarisha uhusiano
wako na si kutegemea kila kitu kutoka kwa mwenza wako.