Mkuu wa mkoa wa Njombe Dkt Rehema Nchimbi akitoa hotuba ya ufunguzi hii leo Novemba 28, 2014
Uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu endapo utaingizwa ajenda ya UKIMWI na wagombea wenyewe, utasaidia kupunguza kasi ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa wananchi
Hayo yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Njombe Mh Dkt Rehema Nchimbi wakati akifungua kikao cha wadau wanaojadili namna ya kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi kilichoandaliwa na tume ya kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) kilichofanyika mkoani Njombe
Dkt Nchimbi amesema suala la kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi ni la Kila mtu hivyo kuwataka wagombea kuingiza ajenda ya Ukimwi katika kampeni zao maana wanaowapigia kura kama hawatakuwa na uelewa namna ya kupambana na maambukizi mapya ya vvu ni kazi bure
Amesema kutokana na maambukizi ya vvu kuwa juu kwa mkoa wa Njombe serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini wamekuwa wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi wote huku akiwataka wananchi kupokea na kutendea kazi yale yote yanayopelekea kupunguza vvu
Dkt Nchimbi ameongeza kuwa anatamani siku moja maadhimisho ya siku ya Ukimwi yasherehekewe kwa furaha, akimaanisha kuwa kusiwepo tena na UKIMWI hapa nchini kwani ni jambo linalowezekana kama kila mmoja atakubali kubadilika
Kwa upande wake Mwenyekiti mtendaji wa TACAIDS Dkt Fatma Mrisho amesema ni kweli Njombe inaongoza kwa maambukizi ya VVU kitaifa, na mwaka huu maadhimisho kitaifa yatafanyikia hapo na kuwaomba wananchi kuonesha mambadiliko ya hali ya juu kupitia maandhimisho hayo
Ametaja baadhi ya makundi yanayochochea ongezeko la maambukizi kuwa ni kuuza ngono, kufanya ngono ya jinsi moja, kuwa na wapenzi wengi kwa wakati mmoja na tena bila kutumia kondomu pamoja na wale wanaotumia madawa ya kulevya kwa kujidunga sindano ama vinginevyo
Amesema makundi hayo yapo kwenye hatari zaidi, na kusema kukua kwa mkoa wa Njombe pamoja na kuwepo kwa fursa mbalimbali ikiwemo mogodi, wananchi watumie fursa hiyo kujiingizia kipato lakini wakumbuke kujilinda na kuchukua tahadhari kuhakikisha hawapati vvu
Dkt Mrisho pia amewataka wananchi kujitokeza kupima na kujua hali zao ili waone ni namna gani watajikinga kwa kuwa tayari watakuwa wanafahamu afya zao
Desemba mosi mwaka huu maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yataadhimishwa kitaifa mkoani Njombe na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete ambapo mkoa huo unaongoza kwa maambukizi ya vvu kwa asilimia 14.8
Washiriki wa kikao hicho.
Picha ya pamoja kati ya mkuu wa mkoa na sekretarieti ya mkoa wa Njombe
Picha ya pamoja na wadau kutoka mkoa wa Njombe
Mwenyekiti mtendaji wa TACAIDS Dkt Fatma Mrisho akizungumza na waandishi wa habari (Picha/habari na Edwin Moshi)