MBUNGE MGIMWA APIGANIA UMEME KALENGA, WANANCHI WAKE WAMPONGEZA‏

MBUNGE wa Kalenga Godfrey Mgimwa (CCM) ameiomba Serikali kupeleka umeme katika vijiji vilivyopitiwa na umeme huku vyenyewe vikikosa Nishati hiyo.

Alitoa ombi hilo wakati akiuliza swali la nyongeza Bungeni ,Mgimwa alivitaja vijiji vilivyopitiwa na umeme ni Kipela kata ya Nzihi,Wenda kata ya Mseke , Tagamenda kata ya Luhota,Stand ya Mbuzi na Migori kata ya Maguliwa. Nguzo  za umeme zikiwa tayari  kata ya Mgama.
Pia Mbunge huyo alitaka kujua Serikali inawaambia nini wananchi wa Vitongoji vya Majengo Mapya   ,Ilala ,godown A na B kata ya Magulilwa ambayo havina nguzo za kutosha.
Akijibu Naibu Waziri wa Nishati na Madini Charles Kitwanga aliwataka wananchi hao kutokuwa na wasiwasi na kusema nguzo zitasambazwa katika maeneo yote.
Vile vile alisema,Serikali inachukua takwimu ya vijiji vyote ambavyo vimepitiwa na umeme wakati vyenyewe havina ili navyo vipate Nishati hiyo. Katika swali la msingi Mbunge huyo alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka umeme katika jimbo la Kalenga kata za Lumuli,Kiwelo ( Kiwele),Ulanda na Magulilwa ili wananchi wa maeneo hayo waweze kuongeza kasi ya maendeleo.
 
Akijibu Kitwanga alisema,kata hizo zimewekwa kwenye utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Umeme vijijini awamu ya pili wa kusambaza umeme  vijijini kupitia ufadhili wa mfuko wa Nishati Vijijini ( REF).

Alisema kazi za mradi huo zinajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 37 .7 ,ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 26.
Mbunge Mgimwa  wa wa nne katikati akikagua mradi wa umeme kata ya Mgama   
Kazi zingine ni ufungaji we Transfoma 12 ,transfoma moja ya kVA 25 ,Transfoma nane za kVA 50 ,Transfoma kVA 100 na mbili za kVA 200 ambapo jumla ya wateja wa awali wapatao 829 wataunganishiwa umeme.

Alisema mradi huo utagharimu kiasi cha sh.bilioni 2.0 na utekelezaji wa mradi unatarajiwa kukamilika kabla ya Juni 2015 huku mkandarasi wa kazi hiyo akiwa ni kampuni ya M/S. Sengerema Engineering Group ya Tanzania.
Kwa upande wao  wakazi wa  Magulilwa na  Kiwere na Ulanda  wamempongeza  mbunge   huyo  kwa  jitihada  zake za  kupigania maendeleo ya  jimbo la Kalenga  likiwemo suala la umeme katika maeneo yao.

Wana CCM Kalenga   wakimpongeza  mbunge  wao Godfrey Mgimwa
Akizungumza na mtandao  huu John Kibiki  kutoka kata ya  Magulilwa  alisema  kuwa wananchi  wa  eneo  hilo  wamefarijika  zaidi na kasi ya  mbunge  wao katika kupigania kata  hiyo  kuwa na umeme na kuwa kwa  kufanya hivyo  kutaongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi wa kata  hiyo.
Huku Anna Sanga mkazi  wa  Kiwere  alisema  kuwa  uwajibikaji wa mbunge  wao ndio ambao  umeendelea  kuwafanya  wana Kalenga   kutoka kimaendeleo na  kuwa  wao  walikuwa hawanajiona kama bado hawajapata  uhuru  kutokana na kukosa  umeme  toka nchi ipate  uhuru wake mwaka 1961.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo