Tatizo
la wanafunzi wa kike kukatisha masomo kutokana na kupata ujauzito
katika wilaya ya kilolo mkoani Iringa Bado ni kubwa ambapo zaidi ya
wasichana 12 wa sekondari wameshindwa kumaliza masomo yao kwa kipindi
cha mwaka jana peke yake.
Hayo yamebainishwa na mkuu wa wilaya ya kilolo Bw Gerald Guninita
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha utengule alipokuwa
akijibu baadhi ya kero za wananchi walizokuwa wakimweleza katibu mkuu wa
CCM Bw Abdulrahman Kinana ambapo amekiri tatizo hilo kuwa linaisumbua
wilaya yake na kuongeza kuwa katika kupambana nalo wametunga sheria
ndogondogo za halmashari na tayari wameshazipeleka kwa waziri mkuu.
Baadhi ya wananchi waliopata nafasi ya kuuliza maswali pamoja na
mambo mengine wameeleza kusikitishwa na kitendo cha serikali kushindwa
kuwachukulia hatua watu wanaohusika na kuwapa mimba wananfunzi hali
inayochangia tatizo hilo kuongezeka kila siku na baadhi ya walimu
wakielezea mazingira magumu wanayofanyia kazi ikiwemo shule kuwa na
vyumba viwili tu vya madarasa ili hali wana wanafunzi kuanzia chekechea
hadi darasa la sita.
Katibu mkuu wa CCM Bw Abdulrahiman Kinana mbali na kueleza mikakati
ya serikali inayoongozwa na chama chake amesema kwa sasa shule za
sekondari za kata zimepiga hatua tofauti na awali na kwamba mchakato
unaoendelea wa kujenga maabara shule zote nchini utainua kiwango cha
elimu kwa kiasi kikubwa, huku katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho
nape nnauye akieleza mikakati kadhaa waliyonayo kwa ajili ya uchaguzi
wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika desemba mwaka huu.