Chama cha waalimu mkoa wa kilimanjaro
(CWT) kinaidai serikali zaidi ya shilingi milioni 985 zilizokatwa kwenye
mishahara ya waalimu kwa miezi miwili hali iliyochangia vyama saba vya
mkoa wa kilimanjaro kushindwa kutoa mikopo kwa waalimu na kuwafanya
watumishi hao kwenda kukopa kwenye taasisi nyingine na kushindwa
kurejesha kwa wakati.
Hayo yamebainishwa na mameneja wa vyama hivyo na kusema kuwa
imekuwa kero kubwa kutokanana vyama hivyo kushindwa kutoa mikopo na
hivyo kusababisha baadhi ya walimu kwenda kwenye taasisi nyingine za
kifedha kutafuta mikopo kwa ajili ya mahitaji yao.
Wamesema zaidi ya walimu 12,000 ambao ni wananchama wa vyama vya
akiba na mikopo wamekatwa mishahara yao na fedha hizo tangu mwezi julai
hazijawasilishwa kwenye saccos hizo hali ambayo inaleta usumbufu mkubwa
kwa Walimu.
Kwa upande wake katibu wa chama cha walimu CWT mkoa wa kilimanjaro
Bw.Nathanael Mwandete ameiomba serikali kuwasilisha fedha hizo kwa
wakati kwa kuwa hali hiyo inaweza kuhatarisha shughuli za ufundishaji
kutokana na walimu hao kufuatilia madai hayo ambayo ni haki yao.
Naye mwenyekiti wa chama cha waalimu (CWT) mkoa wa kilimanjaro
Bw.Omari Mchomvu amesema kama serikali haitalipa madai hayo kwa wakati
chama hicho kitahamasisha walimu kuandamana.