Katika hali isiyo ya kawaida mechi
kati ya Serbia na Albania imeshindwa kumalizika baada ya ndege isiyokuwa
na rubani kubeba ujumbe wa kisiasa kusababisha vurugu zilizowahusisha
wachezaji na mashabiki ndani ya uwanja wa Partizan.
Mechi hiyo ya
kufuzu katika michuano ya soka bara la Ulaya mwaka 2016 ilisimamishwa na
mwamuzi Martin Atkinson kutoka Uingereza katika dakika ya 41 ya mchezo
huo huku matokeo yakisomeka 0-0.
Vurugu ziliibuka wakati bendera
ya Albania na ujumbe kupeperushwa juu ya uwanja na kushikwa na wachezaji
wa Serbia. Wachezaji wa Serbia walijaribu kuichukua bendera hiyo mbele
ya mashabiki kadhaa ilichanika ndani ya uwanja.
'Tukio moja la
kijinga limesababisha vurugu- hiyo ndio njia ya mkato kulielezea tukio
lililotokea usiku' alisema mwandishi wa televisheni ya B92 Milos
Saranovic.
Mwamuzi Atkinson aliwaondoa wachezaji nje ya uwanja na
baada ya kuchelewa kwa dakika 30 Uefa ilithibitisha kusitishwa kwa
mchezo huo.
Serbia na Albania wanahistoria ya kutoelewana mara kwa
mara ikihusishwa na jimbo la zamani la Serbia Kosovo jimbo ambalo
lilijipatia uhuru mwaka 2008.