Kampuni kubwa zaidi ya kuunda
magari, Toyota, imeagiza kurejeshwa kwa magari milioni moja nukta saba
kote duniani kutokana na hitilafu ya breki za magari hayo.
Kampuni hiyo imesema hitilafu tatu zimetambulika kwenye breki katika
miundo mbali mbali za magari ya Toyota ikiwemo muundo wa Lexus.
Magari yaliyo ndani na nje ya Japan yote yameathiriwa na hitilafu hizo.
Hata hivyo kampuni yenyewe imesema haina habari yoyote kuhusu ajali za magari au watu kujeruhiwa kutokana na hitilafu hizo.
Wadadisi wanasema hili ni jambo la kuaibisha sana kwa Toyota ambayo
imelazimika kuagiza magari yake kurejeshwa kiwandani zaidi ya mara moja
kutokana na hitilafu mbali mbali.