UPANDE wa mashitaka kutoka Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wameithibitishia Mahakama ya
Wilaya ya Ilala kwamba aliyetakiwa kuwa shahidi wa pili katika kesi ya
rushwa ya Sh 50,000 inayomkabili Hakimu Grace Kivegele na Karani wake,
Rose Kuhima wa Mahakama ya Mwanzo Buruguri, amefariki dunia.
Katika shauri lililopita Mwendesha
Mashitaka wa Takukuru, Devota Mihayo alidai mahakamani hapo kuwa
aliyekuwa shahidi wa pili katika kesi hiyo, Cresencia Mruma amefariki
dunia, lakini aliomba kuthibitisha kifo hicho.
Hata hivyo, jana upande huo wa mashitaka
ulikuwa na shahidi Rehema Makson (45) ambaye alidai kwamba Aprili 22,
mwaka huu, alipigiwa simu kutoka Kituo cha Polisi cha Tabata
waliomueleza kwamba mtoto wake amekamatwa na kwamba siku hiyo alipelekwa
mahakamani.
Makson alidai siku hiyo alishindwa
kwenda kituoni kwa kuwa alikuwa safarini na kwamba Aprili 23, mwaka huu,
alifika kituoni hapo na kuelezwa kuwa mwanawe amepelekwa mahakamani na
kwamba alikuwa katika Gereza la Segerea.
Alidai polisi wa kituo hicho walimpa
namba ya kesi ambayo ni kesi namba 471/2014 pamoja na jina la Hakimu; na
kwamba siku hiyo hiyo alifika mahakamani na kuomba utaratibu wa dhamana
kwa mshitakiwa.
Akiongozwa na Mihayo, shahidi huyo
alidai alimuomba karani wa Mahakama ya Mwanzo Buguruni amuelekeze jinsi
ya kumpatia dhamana mtoto wake.
Alidai kwamba alitakiwa kuwa na wadhamini wawili na barua mbili zenye picha kutoka katika serikali za mitaa.
Makson alidai Mei 5, mwaka huu, alifika
mahakamani hapo kwa kuwa ndiyo siku ya mshitakiwa kufikishwa mahakamani
kusomewa mashitaka yake, baada ya kesi kuitwa Hakimu Kivegele alimuuliza
kama alikuwa na Sh 50,000 naye alimwambia kuwa hana.
‘’Kwa sababu tulitakiwa kuwa wadhamini
wawili, tulishaurina na ndugu yangu Mruma (sasa ni marehemu) kwamba
twende Takukuru tukapate msaada kuhusu tukio la kuombwa Sh 50,000 bila
ya kusoma barua tulizokuwa nazo,’’ alidai Makson.
Aliendelea kudai kwamba walipofika
katika Ofisi za Takukuru, Ilala, waliambiwa warudi mahakamani na
wamuoneshe barua hizo Hakimu Kivelege na baadaye waliporudi, Mruma
alimuonesha barua hizo Hakimu Kivelege, lakini aliwauliza kama walikuja
wakiwa kamili kwa maana ya kuwa na fedha walizohitaji.
‘’Kwa mara nyingine, tulirudi tena
Takukuru nao walituambia turudi mahakamani hapo siku inayofuata ambapo
Ofisa kutoka taasisi hiyo alimkabidhi Mruma Sh 50,000 ndipo tulienda
mahakamani huku tukiwa na ofisa huyo na kumkuta Hakimu Kivelege akiwa na
kesi nyingine za kusikiliza,’’ alidai.
Shahidi huyo alidai Mruma alionana na
Kivelege na kwamba alielekezwa kuwa fedha hizo ampatie askari; lakini
kutokana na kwamba fedha hizo zilitoka Takukuru hawakuweza kumkabidhi
mtu mwingine.
By Francisca Emmanuel