BASI LA MWAFRIKA LAPATA AJALI MKOANI NJOMBE, ABIRIA WAJERUHIWA NA KUKIMBIZWA HOSPITALI KWA MATIBABU

Abiria zaidi ya abiria 30 wamejeruhiwa vibaya baada ya basi Mwafrika walilokuwa wakisafiria kutoka wilayani Makete mkoani Njombe kweda mkoani Iringa kuacha barabara na kuingia kwenye ukingo wa barabara wakati akikwepa kugongana uso kwa uso na basi la Super Feo

Kwa mujibu wa shuhuda aliyekuwepo eneo la tukio Bw. Linus Matofali amemwambia mwandishi wa eddy blog Riziki Manfred kuwa chanzo cha ajali hiyo ni basi la Super Feo kulipita trekta lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari na ghafla  walikutana barabarani na katika harakati za dereva wa basi la Mwafrika kukwepa kugongana uso kwa uso alihama barabara na kupelekea kuingia ukingonina kisha kubinuka

Ajali hiyo imetokea hii leo majira ya saa nne asubuhi eneo la Kibena nje kidogo ya mji wa Njombe ikilihusisha basi hilo lenye namba za usajili T 726 AGA

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Kibena Dkt. Patrick Msigwa ameieleza eddy blog kuwa hospitali yake imepokea majeruhi 32 ambapo miongoni mwao wanaume ni 15 na wanawake 17 ambao mpaka tunaandika habari hii majina yao hayakufahamika mara moja
 Muonekano wa basi hilo.
Dkt Msigwa amesema mmoja wa majeruhi hao Bi. Jane Chengula mwenyeji wa kijiji cha Makangalawe wilayani Makete alionekana kujeruhiwa zaidi kwa kuvunjika mkono wake mara mbili hivyo anaendelea na matibabu hospitalini hapo na majeruhi wengine wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa lakini wengine wamepelekwa hospitali ya Consolatha Ikonda kwa matibabu zaidi
Aidha mwandishi wetu amesema basi hilo la Mwafrika limeharibika zaidi upande wa kushoto kwa kubondeka na kupasuka vioo

Kamanda wa polisi mkoani Njombe SACP Fulgence Ngonyani amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa dereva wa basi hilo Bw. Furaha Sanga anashikiliwa kwa mahojiano zaidi

Amesema bado chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika mpaka sasa kwa kuwa wanaendelea kumuhoji dereva pamoja na mashahidi wengine ili kubaini chanzo cha ajali hiyo

Kamanda Ngonyani ametoa wito kwa madareva kufuata sheria za barabarani ikiwemo alama zilizopo ili kuepusha ajali kwa kuwa zinaelekeza hali ya barabara ilivyo

Habari/picha na Riziki Manfred Bonzuma, Eddy Blog


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo