Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwahutubia waumini
wa dini ya Kikristu, waliohudhuria katika Sherehe za kuwekwa Wakhfu
Askofu Mteule wa Kanisa la African Inland Dayosisi ya Mwanza, Mchungaji
John Bunango, zilizofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza,
leo.
Makamu
wa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Dk. Mohammed Gharib
Bilal amesema kamwe serikali haitaruhusu mtu yeyote au kikundi cha watu
kuchezea amani iliyopo nchini, kwani amani ya Tanzania ni lulu
inayoliliwa na watu wa mataifa mengine hivyo ni wajibu wa kila mwananchi
kuilinda na kuitunza kwa nguvu zote.
Dk. Bilal ameyasema hayo wakati wa sherehe ya kuwekwa wakfu na
kusimikwa kazini kwa askofu mteule wa kanisa la African Inland Church
dayosisi ya Mwanza, Baba askofu John Binango Mditi, sherehe iliyofanyika
katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na kuhudhuriwa na maelfu ya
waumini wa kanisa hilo, wachungaji na baadhi ya maaskofu kutoka makanisa
mbalimbali nchini, wakiongozwa na askofu mkuu wa kanisa hilo hapa
nchini askofu Silas Kezakubi.
Akihubiri wakati wa ibada hiyo ya kumweka wakfu na kusimikwa kazini
kwa askofu mteule John Bunango, askofu mkuu wa kanisa la African Inland
Church Tanzania ambaye pia ni askofu wa dayosisi ya Tabora Silas
Kezakubi amewaasa vijana kutokubali kutumiwa na baadhi ya watu kuvuruga
amani badala yake watumie nguvu za msuli walizonazo katika kupambana na
adui umaskini.
Akizungumza mara baada ya kuwekwa wakfu, askofu John Bunango Mditi
ambaye anakuwa askofu wa tatu wa dayosisi ya Mwanza, baada ya askofu
Daniel Nungwana ambaye amestaafu baada ya kuhudumu katika dayosisi hiyo
kwa miaka 13, ameiomba serikali kulinda usalama wa maisha ya viongozi wa
dini kutokana na matukio yaliyojitokeza katika siku za hivi karibuni ya
baadhi ya viongozi wa dini nchini kushambuliwa, kujeruhiwa na hata
kuuawa.
Kanisa la African Inland Church dayosisiya Mwanza lilianzishwa
miaka 21 iliyopita. Kanisa hilo hapa nchini hivi sasa linakadiriwa kuwa
na waumini wanaofikia milioni moja na jumla ya makanisa 2,069 kote
nchini, kanisa hilo pia limekuwa chachu ya injili kwa mataifa mengine
kwa kupanua huduma zake nje ya mipaka ya tanzania ikiwemo kuanzisha
kanisa hilo katika nchi ya jamhuri ya kidemokrasia ya congo, burundi na
msumbiji.