REDDS MISS TANZANIA 2014 YAPETA, MAHAKAMA YATOA "GO AHEAD"

Na Mwene Said,Globu ya Jamii

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu,jijini Dar es Salaam, iliamuru mashindano ya urembo Tanzania yaliyopangwa kufanyika Oktoba 11, mwaka huu kuendelea baada ya kutupilia mbali maombi ya dharura yaliyowasilishwa na Prashant Patel dhidi ya Hashimu Lundenga ya kuzuia kuendelea kuendesha kinyang'anyiro hicho kwa madai ya kukiuka mkataba wa makubaliano yao.

Kadhalika mahakama hiyo imesema maombi ya hati ya dharura yaliyowasilishwa na Patel hayana mashiko ya kisheria na kwamba kuzuia kufanyika mashindano hayo ambayo wadhamini mbalimbali wamewekeza fedha zao itasababisha mgangano wa kimaslahi.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Frank Moshi  baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili kuhusu maombi hayo ya dharura ya kuzuia mashindano hayo kufanyika Oktoba 11, mwaka huu.

Hakimu Moshi alisema mlalamikaji amefungua kesi mahakamani hapo pamoja na maombi ya hati ya dharura akiitaka mahakama yake kuzuia mashindano kufanyika kutokana na mlalamikiwa kuvunja haki dhidi ya mwanzilishi mwenzake Patel.

Alisema Patel kupitia hoja za maombi yake, amedai kuwa Lundenga alivunja mkataba huo kwa kufanya mawasiliano moja kwa moja na mawakala bila kumshirikisha.

Hata hivyo, mahakama bila kuacha shaka imeona hakuna sababu za msingi katika hati hiyo ya kusababisha mashindano hayo yasifanyike na kwamba hayawezi kuathiri kesi ya msingi iliyofunguliwa na mlalamikaji huyo.

“Mahakama imeona hakuna sababu ya kuzuia mashindano hayo kwa sababu wadhamini na washiriki wametumia gharama zao na kwamba kwa kufanya hivyo kutasababisha mgongano wa kimaslahi” alisema Hakimu Moshi wakati akitupilia mbali hati hiyo ya dharula.

Akifafanua zaidi alisema hati ya dharura ya mlalamikaji haina mashiko kisheria kwa sababu kesi yake ya msingi ipo mahakamani na kwamba haina uhusiano na mashindano yatakayofanyika Oktoba 11, mwaka huu.

Mapema juzi, mahakama hiyo ilitupilia mbali pingamizi la awali la Lundenga lililotaka hati hiyo ya dharura kutupilia mbali.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo