POLISI mkoani Katavi inawashikilia ndugu wawili wakituhumiwa kumuua
baba yao mzazi, Sado Shija (45) kwa kumcharanga kwa mapanga, wakigombea
mahari iliyotolewa kwa dada yao alipokuwa akiolewa.
Imeelezwa kuwa wanandugu hao, Shinje Italam (25) na Shile Italam (20)
walikuwa na ugomvi na baba yao huyo, wakigombea ng’ombe 20 zikiwa ni
mahari iliyotolewa wakati alipoolewa dada yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kamishina Msaidizi wa Polisi,
Dhahiri Kidavashari amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea
juzi saa mbili na nusu usiku katika kijiji cha Sibwesa, Kata ya Sibwesa,
Tarafa ya Mwese wilayani Mpanda, nyumbani kwa marehemu.
Alieleza kuwa watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani
wakati wowote baada ya uchunguzi wa awali wa shauri lao kukamilika.
Kwa mujibu wa Kidavashari, watuhumiwa hao na mwingine wa tatu ambaye
bado anasakwa na Jeshi la Polisi mkoani humo, wanadaiwa kumuua baba yao
huyo huku wadogo zao wawili mmoja wa miaka 10 na mdogo wake,
wakishuhudia unyama huo.
Akisimulia mkasa huo, Kamanda Kidavashari anadai kuwa usiku huo wa
tukio, marehemu alikuwa amekaa nje ya nyumba yake baada ya kula chakula
cha usiku na watoto wake Mbuke na Ikollo, ghafla alivamiwa na watu
watatu miongoni mwao wakiwa wanawe wawili.
“Watu hao watatu walikuwa na tochi na mapanga walibisha hodi nyumbani
kwa marehemu na kumshambulia kwa mapanga huku watoto wake wadogo wawili
wakishuhudia baba yao akiuawa kikatili,” alieleza Kamanda Kidavashari.
HABARILEO