MFANYAKAZI wa kiwanda cha kutengeneza nguo na vyandarua cha A to Z,
kilichopo Kisongo nje kidogo ya Jiji la Arusha amekufa kwa kile
kinachoelezwa kuwa ni kudondokewa na mashine ya kufungia marobota.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo, ingawa aliahidi kutoa taarifa zaidi leo.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya kiwanda hicho zilizothibitishwa
na Mkurugenzi wa Uzalishaji wa kiwanda hicho, Binesh Haria, zinasema
aliyekufa ametambuliwa kwa jina la Erick Mathayo (25).
Inaelezwa alidondokewa chuma hicho kizito juzi saa 1:00 asubuhi alipokuwa akijaribu kuhakiki moja ya mizigo iliyokwishafungwa.
Mathayo alipasuka kichwa na ubongo kuwa wazi hali iliyoulazimu
uongozi wa kiwanda kumkimbiza hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru
kwa matibabu.
Taarifa kutoka Hospitali ya Mount Meru zilizothibitishwa na mhudumu
wa Kitengo cha Wagonjwa walio katika Uangalizi Maalumu (ICU) ambaye
hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa siyo msemaji wa hospitali, zinadai
kwamba Mathayo alikufa wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi
wa Afya za Wafanyakazi na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA), Ramadhani
Msimbira alikiri kuwepo kwa mazingira anayodai ni mabovu ya utendaji wa
kazi ndani ya kiwanda hicho.
Majira ya saa moja usiku juzi, mwandishi wa gazeti hili alipigiwa
simu na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela akimtaka afike ofisini
kwake ambapo alitii amri hiyo akiwa ameongozana na waandishi wengine
wawili (majina tunayo).
Mongela aliwajulisha kuwa amepigiwa simu na Haria akimwomba awasihi
waandishi wa habari kuacha kuandika habari hiyo kwani itawachafulia kwa
jamii. Hata hivyo, baada ya kupewa taarifa kamili na picha ya tukio hilo
Mkuu wa Wilaya aliwaruhusu waandishi kuendelea na kazi zao kwa
kusisitiza kuwa ''hakuna jinsi ni lazima habari hiyo iandikwe.''
Mwili wa Mathayo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti
katika hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru na mipango ya mazishi
inafanyika nyumbani kwa marehemu Sombetini jijini hapa.