Reyhaneh Jabbari mwenye umri wa miaka 26
amehukumiwa kunyongwa baada ya kukutwa na hatia ya kumuua mtu mmoja
ambaye alifanya jaribio la kumbaka.
Taarifa iliyoripotiwa na CNN
inasema mwanamke huyo amenyongwa katika gereza la Tehrain, Iran ambapo
alikuwa amefungwa baada ya kutenda kosa hilo mwaka 2007 wakati huo akiwa
na umri wa miaka 19.
Mwanamke huyo amekutwa na hatia hiyo
kutokana na kosa la kumuua aliyekuwa mfanyakazi wa wizara ya ulinzi na
usalama nchini Iran, Morteza Abdolali.
Shirika la kimataifa la haki za binadamu Amnesty International limelaani
kitendo cha Iran kutoa hukumu hiyo, ambapo mbali na jitihada ya kampeni
mbali mbali zilizofanywa ikiwemo zile za kwenye mitandao ya kijamii
katika kuipinga hukumu hiyo kuonekana kutozaa matunda.
Taarifa kutoka nchini humo zinasema
mahakama ilitoa hukumu hiyo baada ya kutojiridhisha na utetezi alioutoa
mahakamani kwamba alitenda kosa hilo akiwa anajilinda.
Utafiti wa Umoja wa Mataifa wa mwaka
2011 unaonesha Iran ni moja ya nchi zinazoongoza kwa ukiukwaji wa haki
za binadamu ambapo nchi hiyo ina wastani wa kutoa hukumu ya kunyongwa
mtu 1 kila baada ya masaa 8.