Walinzi wawili wamemkamata mtumishi wa Hospitali ya Wilaya ya
Geita, kwa kile kinachodaiwa kuwa alikuwa akitorosha dawa alizochukua
katika wodi za wagonjwa.
Walinzi hao wa kampuni ya ulinzi ya GSG
walimkamata mtumishi huyo juzi saa 1:00 asubuhi, kwenye lango kuu la
hospitali hiyo alipokuwa akitoka kwenda nyumbani kwake.
Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, George
Rweyemera alisema uongozi wa hospitali unaendelea kuchunguza kujua jinsi
alivyozipata dawa hizo kwa kuwa hahusiki katika kitengo cha dawa.
“Nimeona mnaongea na walinzi pale. Hao wapo chini
ya hospitali. Tunaendelea na uchunguzi kujua huo mzigo ameupataje, yule
mama hahusiki na dawa,” alisema Rweyemera.
“Tukikurupuka tutakosa mengi, kwa hiyo nyie tulieni nitawapa taarifa sahihi zilizokamilika,” aliongeza.
Mfamasia wa hospitali hiyo, Dk Charles Alfred alikiri mtumishi huyo kukamatwa na kwamba dawa hizo alizichukua kwenye wodi.
Dk Alfred alisema kuwa mtumishi huyo aliiba dawa
21 za watoto, mirija 25 ya chupa za maji, cannular 50 za kushikia dripu
za dawa, sindano 100 na chupa 10 za dripu zenye ujazo wa milita 500,
zote zina thamani zaidi ya Sh100,000.
Mlinzi wa kampuni hiyo, Sadick Maganga alisema
juzi saa 1:00 asubuhi alimtilia shaka mama huyo wakati alipokuwa akipita
kwenye lango hilo.
Alisema alikuwa na kikapu alichokitoa nje, kisha akarudi hospitalini akidai kuna kitu amekisahau.
“Aliporudi ili atoke nje ndipo nikamtilia shaka,
nikatoa taarifa kwa msimamizi wangu. Tulipokwenda kuangalia kikapu kile
tukakuta kuna dawa,” alisema Maganga.
Na Salum Maige, Mwananchi
Na Salum Maige, Mwananchi