Mtoto mwenye umri wa siku nane, ameibwa baada ya mama yake kunyweshwa juisi inayosadikiwa kuwa na dawa za kulevya.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Dk. Nassoro Mzee,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mwanamke huyo, Teddy
Bishaliza (19), alilazwa katika Wodi 17 kufuatia afya yake kuathiriwa
na dawa hizo, huku mtoto wake wa kike ikidaiwa kuwa aliibwa katika tukio
lililotokea juzi mtaa wa Chidachi, Manispaa ya Dodoma.
Akizungumza kwa taabu wodini hapo, Bishaliza alisema alijifungua
mtoto huyo Jumatano ya wiki iliyopita hospitalini hapo kwenye Wodi Namba
Tatu na kuruhusiwa kurejea nyumbani na mtoto wake siku iliyofuata.
“Nikitoka wodini, nilikutana na dada ambaye sikuwahi kumuona,
akanisaidia kubeba mizigo michache niliyokuwa nayo na tulipokaa kwenye
benchi akaniambia anikodie bajaj inipeleke nyumbani, tulipofika
hakuteremka kwenye bajaj akaahidi kuja tena kututembelea,” alisimulia
Bishaliza.
Alisema juzi jioni, dada huyo alifika nyumbani kwao akiwa amevaa
dera na kujitanda kikoi kizito chenye rangi ya kijani na chungwa bivu,
baadaye mama yake Bishaliza, alimpelekea chakula kisha akamuacha na
mdogo wake, Rahel Leganga (12), mtoto na mgeni wao huyo.
Rahel alieleza kwamba wakati wakila chakula, mgeni ambaye
baada ya mama Teddy kuondoka alijifungua ushungi aliokuwa amejifunika
sehemu kubwa ya uso wake na kumwagiza ampe vikombe ili awawekee juisi.
“Alitoa juisi ya boksi ile inayouzwa Shilingi 3,000, akanimiminia
dada kikombe cha nusu lita na mimi akaniwekea, nilipoonja nikahisi
chungu nikaikataa, lakini dada akanywa yote,” alisimulia Rahel na
kuendelea:
“Akaniambia ninywe ili niongeze damu mwilini, nikitaka nisisikie
uchungu ninywe haraka haraka kama maji, nikamwambia mimi siinywi,
tulipomaliza kula tu dada akasema anahisi usingizi, akalala.”
Rahel alisema hata yeye baada ya kula na kurejesha vyombo mahala
pake, alilala na alipoamka saa 11:00 alfajiri ya jana, alishangaa
kumkuta dada yake amelala fofofo huku mtoto na mgeni wakiwa hawamo
chumbani.
Alisema baada ya dada yake kuamka, walijaribu kutoka nje, lakini
ilibainika mlango ulifungwa kwa nje, majirani walisaidia kuufungua baada
ya wao kupiga kelele wakiomba msaada, yeye (Rahel) alikwenda kumuita
baba na mama yao wanaoishi mtaa wa pili.
Baba na Mama Teddy wakiwa nje ya wodi namba 17 alimolazwa mtoto wao
huyo, walisema kati yao hakuna anayeweza kumtambua mwizi wa mjukuu wao,
isipokuwa Rahel aliyesema akimuona mwanamke huyo atambua.
Baba Teddy aliyejitambulisha kwa jina la Job Leganga, alilieleza
NIPASHE kuwa Teddy hana mume bali alipata ujauzito na kutokana na
nyumba yao kuwa ndogo, waliamua kumpangishia chumba mtaa wa pili kutoka
nyumbani kwao ili waendelee kumhudumia kwa mahitaji yake muhimu.
Teddy alitaja jina la baba wa mtoto wake kuwa ni Christian Francis,
ambaye hata hivyo, aliondoka mjini hapa na kurejea kwao mkoani
Morogoro.
MAJIRANI WASIMULIA
John Nadoo (50), Mjumbe wa Nyumba Kumi katika eneo analoishi Teddy,
alisema juzi jioni alimuona mwanamke akiwa amevaa dera, amejitanda
mtandio wake kiasi cha kubakiza sehemu ndogo ya sura yake, lakini
hakumsalimia badala yake alionekana akiita watoto.
“Baada ya kuzungumza na watoto, niliona akiongozana na mtoto mmoja,
sikuelewa kilichoendelea mpaka asubuhi nilipopata taarifa kutoka kwa
majirani kuwa mtoto wa Teddy ameibwa jana (juzi) usiku,” alieleza
Nandoo.
Eunice Shaibu (11), alisema: “Aliniita akaniuliza kwa Teddy wapi?”
nikamwambia subiri nikuitie mwenzangu akupeleke mimi nimeachwa nilinde
nyumba, nikamuita Therezia ndiye aliyempeleka.”
Terezia Michael (11), alisema alipofika nyumbani kwa Teddy,
walimkuta akiwa amekaa kwenye kizingiti cha mlango wa kuingia kwenye ua
wa nyumba yao akampokea mkoba.
Rosemary Ndahani (21), anayeishi chumba kilichopakana na Teddy,
alisema akiwa na mpangaji mwenzao, Happy, waliona Teddy akiingia kwenye
ua wa nyumba yao na dada anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 28, mrefu,
mweupe mwenye unene wa wastani, alivaa dera ambalo mtandio wake
aliutumia kujifunga ushungi.
Alisema hawakufahamu kilichoendelea mpaka asubuhi aliposikia Teddy
na mdogo wake wakipiga kelele za kuomba msaada, kufunguliwa mlango wa
chumba chao uliokuwa umefungwa kwa nje na kwamba alipotoka chumbani humo
alikuwa akiweweseka mithili ya watumiaji wa dawa za kulevya.
“Alichokuwa akitamka ni kudai mtoto wake, akisema ‘wameniibia mtoto
wangu, lakini alikuwa hajiwezi, akiweweseka kwa kukosa nguvu kabisa
mpaka wazazi wake walipofika na kumpeleka hospitali,” alieleza Ndahani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alipoulizwa na
NIPASHE kuhusiana na tukio hilo, alisema analifanyia kazi na kwamba
hawezi kuthibitisha kama mtoto huyo ameibwa ama la.
CHANZO:
THE GUARDIAN