Na Daria Erasto
Mtoto wa kike wa miaka 13 aliyenajisiwa na mwajiri wake,
ameeleza kuwa alimtaarifu mke wa mtuhumiwa kuhusu vitendo hivyo, lakini
wawili wakasameheana na kumtaka asiwaambie watu.
Inadaiwa kuwa mtoto huyo aliyekuwa akifanya kazi
za ndani maeneo ya Bunju B, jijini hapa alibakwa zaidi ya mara tatu na
mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 35.
Mtoto huyo, ambaye kwa sasa amelazwa Hospitali ya Mwanayamala, alichukuliwa kutoka Bukoba alikokuwa akiishi na baba yake.
Akihojiwa na Rose Temu, ofisa wa Ustawi wa Jamii
wa Hospitali ya Mwananyamala, mtoto huyo alisema mwajiri huyo alikuwa
akimtendea vitendo hivyo kwa nyakati tofauti, mara ya mwisho ni Jumapili
iliyopita.
Alisema alifika Dar es Salaam Novemba mwaka jana
akitokea Bukoba baada ya kuacha shule akiwa darasa la tano na
kuchukuliwa na mtu huyo kwa makubaliano na baba yake ya kuja kufanya
kazi za ndani.
“Baada ya kuishi kwa muda, siku moja usiku
alinivizia na kuniingilia kinguvu, kisha akaniambia nisiseme. Lakini
nilimwambia mkewe na alipomuuliza, bosi alikataa na kusema mimi muongo,”
alisema.
Mara ya pili aliponifanyia mama alitukuta,
akamuuliza ‘unamfanya nini mtoto wa watu’, akajibu ‘namchezea’.
Wakaingia ndani baadaye mama akasema ameomba msamaha na hatarudia tena
hivyo nisiwaambie watu,” alisimulia.
Mtoto huyo alisema anataka kurudi kwa baba yake
kuendelea na shule, lakini atafanya hivyo baada ya kulipwa Sh160,000
anazomdai za malimbikizo ya mshahara.
Ofisa huyo alisema wamempokea mtoto huyo kutoka
kwa polisi Jumanne na tayari ameshafanyiwa vipimo mbalimbali. Alisema
atakuwa chini yao hadi watakapowasiliana na wazazi wake.
Mjumbe wa Mtaa wa Bunju B, Josephat Rutayuka
alisema Jumapili ya saa 12:00 asubuhi, mtoto alikwenda kumlalamika
kuhusu vitendo viovu.