MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone
juzi alilmtaka mshereheshaji katika warsha ya wadau wa rasimu ya mpango
wa usimamizi na uendelezaji wa pamoja wa rasilimali za maji Bonde la
Kati kuacha kuendesha utambulisho wa wajumbe hao kwa lugha ya Kiingereza
badala yake atumie Kiswahili.
Alilazimika kuingilia kati baada ya
kushuhudia baadhi ya wajumbe waliokuwa wakitambulishwa na kutakiwa
kusimama ili waonekane kushindwa kufanya hivyo kwa kile kilichodhihirika
wazi kupigwa na bumbuwazi na utambulisho huo wa lugha ya Kiingereza.
Akionesha wazi kukerwa kwake na
mshehereshaji, Dk Kone alisema wakati taifa liko katika juhudi za kukuza
Kiswahili, baadhi ya Watanzania wanakwamisha juhudi hizo kwa sababu
hafifu kama za kuwepo baadhi ya washiriki wasiojua Kiswahili.
“Wajumbe wa warsha hii wako 200 na
wasioelewa Kiswahili ni wanne tu. Idadi hii ndogo haiwezi kusababisha
mkutano huu uendeshwe kwa Kiingereza. Wengi wetu hapa japo tunajua
Kiingereza, baadhi yetu mwaka umepita bila kukizungumza; hivyo inahitaji
mtu kujiandaa ili kuwa katika nafasi nzuri ya kukizungumza,” alisema.
Aidha, alisema endapo warsha hiyo
ingeendeshwa kwa lugha ya Kiingereza, wachangiaji wa rasimu hiyo
wangekuwa wachache hivyo kuwanyima wengi fursa ya kutoa mawazo yao.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mkuu
huyo wa Mkoa aliwataka wadau kushirikiana katika kukabiliana na
changamoto mbalimbali zinazokabili usimamizi wa rasilimali za maji
kutokana na suala hilo kuwa mtambuka.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni migogoro inayohusu maji pamoja na siasa.
Alisema Sekta ya Maji ina jukumu kubwa
katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, lakini kwa bahati mbaya
inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo bila kutatuliwa huathiri
utekelezaji wa mipango na mikakati ya maendeleo na usimamizi wa
rasilimali za maji.
Bonde la Kati lenye makao yake makuu
mkoani Singida ni miongoni mwa mabonde tisa yaliyopo nchini na
linajumuisha maeneo ya Dodoma, Manyara, Singida, Tabora, Shinyanga,
Arusha na Kilimanjaro ambapo linagusa jumla ya wilaya 26. Ni la pili kwa
ukubwa likiwa na kilomita za mraba 143,099.